Jan 17, 2017

Serikali Yamalizana Na Wenyeviti Wa Serikali Za Mitaa, Yawaruhusu Kutumia Mihuri Yao

Baada ya mvutano wa muda mrefu baina ya Serikali na Wenyeviti wa Serikali za mitaa,Serikali imesitisha muongozo wake wa kuzuia kutumia mihuri kwa wenyekiti wa serikali za mitaa.

Akizungumza leo hii Jijini Dar es salaam na wawakilishi kutoka serikali za mitaa, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simba Chawene amesema amesitisha muongozo uliotolewa juu ya utumiaji wa mihuri kwa Wenyeviti wa serikali za mitaa mpaka hapo baadae itakapojadiliwa tena.

''Hakukuwa na dhamira yeyote ya kupunguza mamlaka ya heshima yenu Wenyeviti, lakini kama mihuri inaweza kupunguza heshima yenu nimeona kufuta muongozo huu Mpaka pale tutakapo jadili tene upya swala hili" amesema

Sanjari na hayo Waziri Simbachawene amefafanua kuwa kulikuwa na sababu za msingi za kutoa muongozo huo wa kutokutumia mihuri kutokana na matumizi mabaya ya mihuri kwa Wenyeviti wa serikali za mitaa na kupelekea kuigawa ardhi bila utaratibu maalumu.

Hata hivyo Katibu wa Wenyeviti Mkoa wa Dar es salaam Mariam Machicha ameishukuru Serikali kwa kuona tatizo hilo na kuahidi kulifanyioa kazi.
Share:

Kilichotokea Hadi Kupelekea Kukamatwa Kwa Edward Lowassa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, limemkamata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Lowassa ambaye pia alikuwa mgombea urais wakati wa uchaguzi mkuu mwaka juzi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amekamatwa mjini Geita jana muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Mkoa wa Kagera alikokuwa kwa shughuli za kisiasa.

Mbali na Lowassa, viongozi wengine waliokamatwa ni Profesa Mwesigwa Baregu na Hamis Mgeja.

Lowassa na wenzake hao, walikuwa wakielekea Kata ya Nkome, Jimbo la Geita Vijijini kushiriki mkutano wa kampeni za udiwani.

Tukio hilo lilitokea jana saa 9:20 mchana baada mwanasiasa huyo kuwasili mjini Geita na kukuta wananchi wengi wakiwa wamejaa barabarani wakitaka awasalimie.

Kutokana na umati mkubwa wa watu waliokuwa barabarani, Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, yeye na msafara wake walilazimika kuingia eneo la stendi ya zamani ya mabasi kuwasalimia wananchi hao.

Hata hivyo, kabla hajaanza kuzungumza na wananchi hao, magari matatu yaliyokuwa yamejaa askari polisi yalifika mahali hapo na kumkamata.

Baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita na kukaa kwa dakika kadhaa, Lowassa na wenzake walihamishiwa ofisini kwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo kwa mahojiano.

 MABOMU YA MACHOZI

Baada ya mwanasiasa huyo kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, kundi la wananchi wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, walianza kueleka maeneo ya kituo hicho ili kujua kinachoendelea.

Wakati wakielekea katika eneo hilo, polisi walilazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi yaliyoathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi Mseto.

 WAANDISHI WAPIGWA

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya waandishi wa habari walijikuta wakiwa katika wakati mgumu wa kufanya kazi zao baada ya kukamatwa na kupigwa na polisi.

Miongoni mwa waliopigwa ni Mwandishi wa Habari wa Chanel Ten, Vales Robert na Joel Maduka wa Stom Radio.

Akizungumzia tukio hilo, Robert alisema yeye na mwenzake walipigwa baada ya kushutumiwa na polisi, kwamba walikuwa wakipiga picha za tukio la Lowassa kukamatwa.

“Tulivamiwa na polisi wakati tukipiga picha na wakati tunapigwa, tulikuwa tumevaa vitambulisho vyetu vya uandishi wa habari.

“Yaani wamenivunjia kamera yangu, lakini nashukuru sijaumia sana,” alisema Robert.

 KAMANDA WA POLISI

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita, Mwabulambo, alipopigiwa simu kuhusu suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake ambaye alisema alikuwa katika kikao na Lowassa.

“Mimi ni mlinzi wa afande RPC, samahani yupo kwenye kikao na mheshimiwa Lowassa, nakuomba umtafute baadaye,” alisema bila kutaja jina lake.

Kutokana na tukio hilo, viongozi mbalimbali wa Chadema Mkoa wa Geita, walikuwa katika ofisi za Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita ili kujua hatma ya tukio hilo.

Kukamatwa kwa Lowassa na wenzake hao ni mwendelezo wa viongozi wa Chadema kukamatwa baada ya Januari 14, mwaka huu, Jeshi la Polisi, Mkoa wa Geita kumkamata Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Geita, Upendo Peneza.

Mbunge huyo baada ya kukamatwa, aliunganishwa kwenye kesi ya uchochezi na Diwani wa Kata ya Kasamwa, Fabian Mahenge wakituhumiwa kufanya uchochezi huo Januari 6, mwaka huu katika mkutano wa hadhara.

Kabla ya kumkamata Peneza, polisi waliwakamata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika na Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Kagera, Conchesta Rwamlaza, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Anna Rose.
Share:

Mbeya: Maiti iliyozikwa yakutwa chumbani kwenye godoro.

Wakazi wa Isanga Jijini Mbeya wamekumbwa na taharuki baada ya tukio lisilo la kawaida ambapo maiti iliyokwenda kuzikwa katika makaburi ya zamani ya Isanga ilikutwa ikiwa kwenye godoro ndani ya nyumba alimofia.

Taarifa yaJeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya inasema kuwa tukio lilitokea mnamo tarehe 16.01.2017 majira ya saa 4:30 asubuhi katika mtaa wa Igoma “A”, Kata ya Isanga, Jijini Mbeya.

Kufuatia taarifa hiyo Polisi walifuatilia na kubaini kuwa tarehe 16.01.2017 majira ya saa 1:00 asubuhi mtu mmoja aitwaye JAILO KYANDO na mke wake aitwaye ANNA ELIEZA wote wakazi wa mtaa wa Igoma “A” waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa kwanza aitwaye HARUN JAILO KYANDO amefariki dunia akiwa amelala.

Taarifa za awali zinadai kuwa marehemu tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa hali iliyopelekea kuishi nyumbani pasipo kusoma.

Kufuatia kifo hicho msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika. Majira ya saa 6:00 mchana jeneza lililetwa msibani na kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa na blanketi na kulazwa chini kwenye godoro, baada ya maombi yaliyoongozwa na walokole waitwao BONDE LA BARAKA vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha jeneza kuzikwa.

Waombolezaji waliporudi nyumbani walitaharuki kuona mwili wa marehemu mtoto HARUN JAILO KYANDO ukiwa chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.

Kutokana na hali hiyo taarifa zilifikishwa Polisi mara moja, askari Polisi walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu ambao kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Taratibu nyingine za mazishi zitafanyika leo tarehe 17.01.2017. Mpaka sasa bado haijafahamika ni uzembe /bahati mbaya wafiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza au kulikuwa na hujuma zozote.

Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili.
Share:

Kilichompata Mchungaji aliyetabiri kifo cha Rais Robert Mugabe

Mwishoni mwa mwaka 2016, raia na wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe waliandamana kupinga utawala wa Rais Robert Mugabe ambaye amekuwa madarakani tangu 1980.

Habari zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa zimedai kuwa maafisa wa polisi nchini Zimbabwe wamemkamata  mhubiri aliyetabiri kwamba Rais Robert Mugabe atafariki mwezi Oktoba mwaka huu.

Pastor Patrick Mugadza alikamatwa akiwa mahakamani mjini Harare Jumatatu ambapo alikuwa ameenda kwa kesi nyingine dhidi yake. Wakili wake Gift Mtisi amewambia waandishi wa habari kuwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kuvalia bendera ya taifa

Wakili wake ameimbia AFP kuwa; "Alikuwa amefika mahakamani kwa kesi hiyo polisi walipomkamata wakati wa mapumziko na kumfungulia mashtaka kwa sababu ya unabii huo"

Awali alishtakiwa kwa kukosea heshima mamlaka ya Rais lakini shtaka hilo likabadilishwa baadaye na kuwa amewatusi watu wa asili fulani au dini fulani.

Pastor Mugadza wiki iliyopita aliandaa kikao na wanahabari ambapo alitabiri kwamba Mugabe atafariki Oktober 17 mwaka huu.
Share:

Waziri Nape Kawajibu Waliobeza Diamond Platnumz Kukabidhiwa Bendera Ya Taifa.......Ridhiwan Kikwete Hajataka Kukaa Kimya, Kamjibu Tena Nape

Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Tanzania Nape Nnauye sio kwamba hakuona maoni ya Watanzania kwenye mitandao ya kijamii baada ya yeye kumkabidhi bendera mwimbaji wa bongofleva Diamond Platnumz kwenda Gabon kwenye michuano ya Afrika.

Waziri Nape ameziona comments za Watanzania na yeye amewajibu baada ya Diamond kuhudhuria kwenda kutumbuiza kwenye mashindano hayo ya soka Afrika yanayofanyika Gabon ambapo Nape baada ya kuona imekua gumzo mitandaoni yeye kumpa Diamond bendera.

Kupitia Twitter  yake Waziri Nape alichukua picha ya Diamond akiwa na wengine wa Afrika walioziwakilisha nchi zao kwenye mashindano yao wakiwa na bendera na kuandika

"Ulizeni tena kwanini nilimkabidhi bendera Diamond"

Kwa sababu mjadala umekua mrefu sana kupitia twitter,baada ya post ya Waziri Nape kwenye watu walioandika tena ni Mbunge Ridhiwani Kikwete ambaye ameandika: Nafikiri Waziri amepanik kutokana na mashambulizi lkn ukweli ni kuwa tunahitaji kushiriki afcon 2019

Share:

EDWARD Lowassa Kaachiwa Huru....Mashuhuda Waeleza Jinsi Alivyokamatwa

Waziri mkuu Mstaafu na Mgombea wa Urais 2015 kupitia CHADEMA, Edward Lowassa leo alikamatwa na jeshi la Polisi  wakati akiwa anaenda kwenye kampeni za uchaguzi Kata ya Nkome na baadaye aliachiwa  huru ambapo taarifa za polisi zinadai kuwa walimzuia kwa sababu za kiusalama.

Kupitia kituo cha Television cha Azam wameripoti habari ya kukamtwa kwa Lowassa ambapo baadhi wa wananchi wameeleza ilivyokuwa.

"Tulikuwa kwenye msafara ya kumpokea Lowassa lakini tulipofika hapa stendi wananchi walitaka kuongea na Lowassa, kabla hata hajashuka kwenye gari askari walituvamia wakasema tuondoke moja kwa moja twende kituoni"- shuhuda

Sikiliza mkasa mzima hapo chini
Share:

Waziri Tizeba amjibu Zitto kuhusu chakula

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amefunguka na kumjibu mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Zitto Kabwe kuhusu hali ya chakula nchini na kusema kuwa alikurupuka kwani kile alichokisema hakina ukweli wowote

Waziri Tizeba amesema kuwa nchi ilikuwa na chakula cha kutosha hivyo hakukuwa na haja ya NFRA kuongeza chakula kingine kwani kulikuwa na ziada ya chakula tani milioni tatu.

"Yupo mtu mwingine alikurupuka na kusema jamanii Tanzania imebakiza chakula cha siku nane, sasa hivi ni wiki ya tatu inakwenda ya nne watu bado wanakula, na hatujatoa chakula huko NRFA hata kilo moja, harafu nisemee suala la kuwa na akiba ya tani 90,000  hii nchi ina mavuno makubwa ina ziada ya tani milioni tatu hivyo kwanini NRFA wakanunue tani zingine milioni moja ili iweje. Tulikuwa na tani zaidi ya milioni tatu za ziada NRFA wangeenda kununua tani elfu moja au elfu tisini au laki tatu za nini? Alihoji Waziri wa Kilimo

Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia tiketi ya ACT Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe mnamo tarehe 3 ya mwezi Januari kupitia ukurasa wake wa Facebook alitoa taarifa juu ya hali ya chakula nchini na kusema chakula ambacho kilikuwepo kwenye ghala ya Taifa ya chakula kilikuwa ni chakula cha kutosha siku nane tu pekee.

Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu (BOT) ya mwezi Novemba 2016 ilionesha kuwa ghala la Taifa la chakula NFRA lilibakiwa na tani 90,000 tu za chakula.

"Ghala la Taifa lina hifadhi ya chakula kinachotosha siku 8 tu ikitokea dharura yeyote. Novemba 2015 kulikuwa na chakula cha kutosha miezi 2. Taarifa ya Benki Kuu ya mwezi Novemba inaonyesha kuwa NFRA imebaki na tani 90,000 tu za chakula". Aliandika Zitto Kabwe
Share:

Jan 16, 2017

YALIYOJIRI Kwenye Kesi ya Maxence Melo Mahakamani Kisutu

Kesi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media, Maxence Melo iliyokuwa isikilizwe Jumatatu hii katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imeahirishwa hadi Februari 16 mwaka huu kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.

Uamuzi huo umetolewa na Wakili wa Jamhuri kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na haujakamilika bado, hivyo hakimu anayeendesha kesi hiyo Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Victoria Nongwa aliutaka upande wa Jamhuri kukamilisha haraka upelelezi wa kesi hiyo ili iweze kusikilizwa tarehe iliyotajwa.

Kwa mujibu wa mtandao huo, Maxence Melo anashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao na Kusajili tovuti ya JamiiForum kwa kikoa cha .com badala ya .co.tz jambo ambalo inadaiwa ni kinyume cha sheria.
Share:

ASKOFU Pengo Ayataka Makanisa Kutoshindana Kumtumikia Mungu

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ametoa wito kwa makanisa kutoshindana kumtumikia Mungu.Wito huo umetolewa na askofu huyo Jumapili hii wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Rita wa Kashia, Temboni jimboni humo.

“Tusiingiwe na moyo wa kiburi tukajiona bora kuliko waumini wa parokia nyingine, kwa sababu katika muda mfupi mmefanya makubwa. Kuna watu katika jumuiya zetu wakitambua wewe ndio mkuu, hatari ya kujigamba na kujidai ni kubwa kwamba ni kwa nguvu zako unafanya hayo unayofanya, tukumbuke ukuu unatoka kwa Mungu ndio unaodumu lakini wa binadamu ni ukuu wa kupita,” alisema Pengo.

Aidha Askofu Pengo aliwataka waumini wa makanisa kumtanguliza Mungu mbele na hata kama kuna mambo makubwa wanayafanya, wasijigambe kwa kujilinganisha na makanisa mengine ambayo hayajaweza kufikia walipo, bali kumshukuru Mungu daima kuwafikisha walipofika
Share:

Rais Magufuli Ateua Wabunge Wapya Wawili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 16 Januari, 2017 amefanya uteuzi wa Wabunge wawili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi mmoja.

Abdallah Bulembo (Kushoto) akiwa na Rais Magufuli
Wabunge walioteuliwa ni Alhaji Abdallah Majula Bulembo na Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.

Wabunge wateule hawa wataapishwa kwa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Abdallah Bulembo ndiye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na pia alikuwa ni mujumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kabla ya majukumu ya kuendesha kampeni urais mwaka 2015 zilizomuingiza Rais Magufuli madarakani.

Kwa upande wake Prof Kabudi, ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria, lakini kilichong'arisha zaidi ni pale alipoteuliwa na Rais Kikwete kuwa mmoja kati ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mst. Joseph Sinde Warioba.

Prof. Kabudi amekuwa mahiri katika mihadhara mbalimbali kitaifa, hasa wakati ule wa mchakato wa Katiba Mpya.

Prof Paramagamba Kabudi
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Benedicto Martin Mashiba kuwa Balozi.
Kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi Mteule Benedicto Martin Mashiba itatangazwa baadaye.

Share:

Trending News

Copyright © Siasa Huru | Powered by Blogger Design by JK | Blogger Theme by JR