• Breaking News

  May 8, 2016

  Barua ya wazi kwa John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano Tanzania.


  Nianze kwa kusema wewe, Rais Magufuli ni binadamu na hakuna binadamu mkamilifu asiye na mapungufu, hiyo ni sifa ambayo Muumba wetu pekee anayo na anastahili kuwa nayo.

  Mimi Mag3, nina hakika 100% kwamba nakusaidia Magufuli kuliko wanafiki wanaoshinda mitandaoni wakikusifia hata pale inapotakiwa uambiwe, hapana Mkuu, hapa umejikwaa.

  Naamini Rais unasukumwa na nia ya dhati ya kuwasaidia ndugu zako Watanzania waondokane na matatizo yaliyoliandama taifa letu kama kupe kwa nusu karne toka tupate uhuru.

  Katika misingi hiyo nina hakika kwamba Rais unafuatilia ukosoaji wetu ukijua unakusaidia katika kujua kwa nini wengine wetu tulikunyima kura na tulifanya hivyo kwa kusukumwa na nini.

  Kila mtu anajua fika kwamba kuitoa CCM madarakani kwa Katiba tuliyo nayo ni ndoto, hata hivyo bila kujali maslahi binafsi, tuliwapigia kura wapinzani kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

  Tulifanya hivyo tukijua juhudi zitakazotumiwa na chama tawala kuhakikisha ndoto zetu zitabaki ndoto kwani uhuru na haki ni vitu viwili adimu sana katika msamiati wa CCM.

  Wapo waliatanguliza maslahi binafsi na kwa tamaa ya ajira serikalini, mafanikio kibiashara na kitaaluma, walikupigia kura wakitegemea upendeleo kiitikadi katika teuzi mbali mbali.

  Watu kama hao kamwe hawawezi kupata ujasiri wa kukuambia ukweli na kwa kuwa wengi ni wa chama chako, watakusifu mchana huku usiku wakilalama walivyo na wasiwasi nawe.

  Wengine hatuko hivyo, hakuna tunachotaka kwako bali utawala bora unaotoa uhuru na haki kwa wananchi wote bila kujali kabila, jinsia, rangi, itikadi...yote kama yalivyooanishwa ndani ya Katiba.

  Hivyo hatutasita kuita koleo kwa jina lake kama tutahisi hatutendewi haki kwa kufuata sheria na kwa bahati wote tunakubaliana kwa jambo moja la msingi...kutanguliza maslahi ya kwa taifa.

  Tunajua kwamba watendaji wote wakuu waliotufikisha hapa tulipo ama walikuwa ni viongozi wa CCM na serikali yako kwani ndio wamekuwa waamuzi wa hatma ya nchi miaka yote.

  Hivyo inajulikana wazi kuwa kama majipu yapo, ama yapo tele ndani ya chama chako au ndani ya serikali yako na yaendelee kutumbuliwa tu hata kama mengine yapo sehemu nyeti.

  Tatizo linakuja pale majipu yanapokushangilia ukitumbua majipu, ni jukumu ketu kukushtua uwe mwanagalifu na huo ushangiliaji kwani hakuna namna unaweza kuwa kwa nia njema.

  Tukikosoa tunaitwa maadui lakini kwa ukweli sisi tunafanya hivyo kwa nia njema tu na hapa tunasisitiza nia ni kukusaidia kiutekelezaji kuliko inavyopotoshwa na wanafiki waliokuzunguka.

  Huna haja ya kutuogopa kama nia yako na yetu tunaokukosoa ni moja...kuliona taifa linanusurika kutoka lindi la umasikini...achana kabisa na wanafiki, ungana na wananchi wa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku