• Breaking News

  May 2, 2016

  Chama cha Wasiomwamini Mungu Chapigwa Marufuku

  Wakenya wasiomwabudu Mungu walipata pigo Jumamosi baada ya Mwanasheria Mkuu, Prof Githu Muigai kuharamisha chama chao.

  Hatua hiyo ilitokea siku moja tu baada ya viongozi wa kidini kutoa wito kwa Prof Muigai kujiuzulu kwa kusajili muungano huo mwanzoni mwa mwezi Aprili.

  Kwenye taarifa iliyotolewa na afisi ya Mwanasheria Mkuu, hatua ya kufutilia mbali muungano huo ilitokana na malalamishi mengi ambayo yalikuwa yanatolewa na mashirika tofauti mbali na viongozi wa kidini.

  “Kutokana na kupokewa kwa maoni mbalimbali katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu kutoka kwa viongozi mbalimbali wa dini na mashirika mengine kuhusu kusajiliwa kwa Chama cha Wasioamini Mungu cha Kenya, Mwanasheria Mkuu ameagiza Msajili wa Vyama vya Kijamii afutilie mbali mara moja usajili huo,” ikasema taarifa hiyo.

  Iliongeza kuwa uamuzi umetolewa kwa msingi wa Ibara 12(1)(b) ya sheria ya vyama vya kijamii hadi wakati Mahakama ya Juu itakapoamua kuhusu uhalali wa chama hicho na ikiwa kinalingana na katiba.

  Viongozi wa kidini Ijumaa walimtaka Prof Muigai ajiuzulu, huku wakisema usajili wa chama hicho ulikiuka katiba.
  Kulingana na Muungano wa Kitaifa wa Makanisa ya Kipentekosti (KNCPCM), katiba inatambua ukuu wa Mungu kwa hivyo ni kinyume kusajili chama cha wasioamini Mungu.

  Naibu mwenyekiti wa muungano huo Askofu Stephen Ndichu alisema Mwanasheria Mkuu hataki kutambua masuala ya dini humu nchini.

  Shinikizo
  “Tunatamka Mwanasheria mkuu afutilie mbali usajili wa chama hicho la sivyo tutaenda kortini kutaka kifutiliwe mbali kwa kuwa kilisajiliwa kinyume na sheria,” akasema Bw Ndichu.

  Viongoi hao wa dini walikuwa wamepanga kuleta pamoja waumini wa dini tofauti wakiwemo Waislamu na Wahindi ili waungane kufanya maandamano makubwa kulalamikia hatua ya kusajiliwa kwa chama hicho.

  Chama cha wasiomwamini mungu kilisajiliwa Februari 17, kisha cheti kikatolewa rasmi kwa mwenyekiti wao Bw Harrison Mumia Aprili 7.

  Wakati huo, Bw Mumia alisifu hatua hiyo na kusema ilikuwa hatua nzuri ya kuhakikisha serikali inatambua Wakenya wote kwa kiwango sawa licha ya imani yao.

  Chanzo: Swahili Hub

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku