• Breaking News

  May 31, 2016

  Hatuhitaji Elimu ya Darasani Kuepuka Ajali za Mabasi ya Mwendo Kasi

  Mazoea hujenga tabia. Sitaki kuamini kuwa hiki kinachotokea juu ya hizi ajali zinazohusisha magari ya mwendo kasi kinahitaji hata elimu ya darasani.

  Ni muda mfupi sana tangu mabasi ya mwendo kasi yaanze kazi ya kusafirisha abiria ndani ya jiji la Dar es Salaam lakini mpaka sasa ni zaidi ya ajali tatu zimeshatokea ikiwemo ya kifo cha mtoto mdogo, ajali ya bodaboda na gari la mwendo kasi na nyingine ile iliyotokea juzi maeneo ya Magomeni, gari dogo aina ya Toyota Vitz kuingia kwenye barabara ya mabasi hayo na kuligonga gari la mwendo kasi.

  Kama nilivyoanza kwa kusema mazoea hujenga tabia ndicho nachokiona hiki kinachoendelea sasa. Mabasi ya mwendo kasi yametengewa barabara zake za kupita lakini bado madereva wa bodaboda na watembea kwa miguu wanaendelea kupita kwenye njia hizo huku wakijua kabisa hawaruhusiwi kufanya hivyo lakini pia wanakuwa wanahatarisha maisha yao.

  Hatuhitaji kurudi darasani kujifunza hili, yatupasa kufuata taratibu zilizowekwa ili kupunguza ajali za barabarani. Nimezidi kujiuliza kama hili dogo linatushinda, je itakuwaje ile teknolojia mpya ya mabasi ya kusafirishia abiria walioigundua nchi ya China ikifika kwetu kila siku watu si watakufa kwa ajali hiyo.

  Kinga ni bora kuliko tiba. Tukiamua kufuata sheria na utaratibu uliowekwa ni dhahiri tutaweza kuondoa ugonjwa huu ulioanza wa ajali za mabasi ya mwendokasi.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku