• Breaking News

  May 28, 2016

  Jumuia ya Afrika Mashariki yavunjika Baada ya Miaka 10

  JUMUIA ya Afrika ya Mashariki ya sasa ni marudio ya Jumuia ya Afrika Mashariki iliyoanzishwa kwa furaha mwaka 1967 na kuvunjika kwa uhasama mwaka 1977 – ikiwa ni baada ya kupita miaka kumi tu.

  Ushirikiano huo ulitokana na undugu wa nchi husika – Kenya, Tanzania na Uganda – zilizokuwa makoloni ya Uingereza,  ambao ulichipuka kwa furaha kubwa miongoni mwa wananchi wa mataifa haya matatu, kabla ya kuvurugwa na wanasiasa waliokuwa wakitawala nchi hizi kwa kujali zaidi maslahi yao ya kisiasa badala ya wananchi.

  Waasisi wa ushirikiano huo ambao leo hii wote hawapo, ambao ni Jomo Kenyatta, Julius Nyerere na Milton Obote,  walijikuta katikati ya miali ya moto ya kisiasa ambayo iliwatenga katika kambi za kisiasa na kiuchumi, yaani ubepari na usoshalist (au ujamaa).

  Kwa waliokuwepo wakati wa jumuia hiyo,  moja ya jumuia zenye ustawi mkubwa kimkoa duniani,  walishuhudia  ushirikiano wa kweli wakati huo katika nyanja hususan za kiuchumi zilizojumuisha usafiri wa anga, reli, mawasiliano, ushuru na kadhalika, mambo yaliyowanufaisha  wananchi wake kikamilifu.

  Wakati huo Mtanzania aliweza kusafiri kwa treni au ndege kwenda Kenya ama Uganda bila hati yoyote na  akaitumia fedha yake ya Tanzania huko Uganda na Kenya bila kuibadilisha.  Pia, mtumishi wa taasisi za Afrika Mashariki  aliweza kuhamishwa kutoka Nzega na kupelekwa Mombasa na kadhalika.

  Ulikuwa ni ushirikiano wa kweli ambao kwa walioushuhudia wana mashaka kama utarejea tena, na ukirejea, basi ni baada ya makumi ya miaka.

  Moto wa kuunda nchi moja na serikali moja miongoni mwa viongozi hao watatu wa mwanzo, uligeuka na kuwa shubiri ya kisiasa ama kwa kuingiliwa zaidi na ‘mawazo’ kutoka nje au uchoyo wa wanasiasa haohao waliohisi maslahi yao kisiasa na kiuchumi yangetoweka.

  Siasa za Vita Baridi zilizokuwa zikiongozwa na Marekani na Urusi duniani, chini ya ubepari na ujamaa, zikaitoa mhanga jumuia hiyo.

  Pia, kuingia madarakani kwa Iddi Amin wa Uganda mwaka 1971 baada ya kumuondoa Obote aliyekuwa rafiki wa Nyerere, na Nyerere kukataa kukaa naye meza moja, kuliongeza mkanganyiko  wa kuidhoofisha jumuia hiyo ambapo  mwaka 1977 ilivunjika kwa uhasama wa “hali ya chini” na hatimaye kila mtu kuchukua chake.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku