• Breaking News

  May 6, 2016

  Kwenye Hili la Sukari Rais Wangu Sikuungi Mkono, Uchumi ni Kanuni Siyo Amri!

  Ni dhahiri kumekuwa na mayowe mengi ya walalahoi na kuishi hai wakishangilia kauli ya Mhe. Rais Magufuli juu ya kuvamia magodown ya wafanyabiashara na kutaifisha sukari ya wafanyabiashara ili kushinikiza uimara wa soko.

  Kwangu mimi hii ni sawa na kukata miti kwenye chanzo cha chemichemi kwa madai kwamba miti hiyo haitoi mchango wa maji ya kutosha katika mkondo wa maji. Mimi nadhani kwa busara zaidi mtaalamu wa mazingira angehitaji aidha kupanda miti zaidi au kuongeza mbolea, dawa na usimamizi kwa miti iliyopo ili mkondo wa maji uzidi kukua.

  Sasa najiuliza, ni nini mantiki ya haki ya kumiliki mali kwa mujibu wa serikali ya awamu ya tano. Mwalimu wangu wa falsafa alikuwa anapenda kunena yafuatayo:
  "Waafrika wengi ni wabobezi kutibu dalili za ugonjwa na siyo ugonjwa wenyewe".

  Nani haelewi hali ya uchumi wa nchi hii sasa hivi? Nani hajayaona mabonde makubwa yenye rutuba inayoweza kutumika kuzalisha mazao mengi ikiwamo miwa na kulitatua tatizo la upungufu wa sukari kwa kanuni ya kiuchumi badala ya amri?

  Nani hajui kwamba wakulima wetu wanalima kimazoea pasipo kufuata utalaamu wowote huku somo la kilimo likipewa kisogo mashuleni na vyuoni?
  Sasa kama hali iko hivi, utakapomaliza kupokonya sukari ya wafanya biashara utapokonya nini tena?

  Biashara ya sukari ni kama biashara nyingine wala hauhitaji nguvu bali maarifa-

  CONSIDER SUPPLY AND DEMAND AS YOUR PROSPECTIVE TOOL TO CONTROL YOUR MARKET.

  Siamini kama Tanzania ya viwanda uliyotuahidi ni hii ya kupokonyana sukari, tengeneza misingi imara itakayowakomboa wakulima, vijana wasaka ajira na wawekezaji kwa ujumla.

  Katika hili nimeamua kufuata njia ya Mark Twain kwamba 'uzalendo siyo kuiunga serikali kila wakati bali kuiunga mkono nchi kila wakati na kuiunga mkono serikali pale inapostahili tu'.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku