• Breaking News

  May 17, 2016

  Majaliwa Asema Serikali inataka Watu Wake Wafanye Kazi Ndiyo Maana Wamezuia Matangazo ya Bunge live

  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa serikali kuzuia matangazo ya live ya bunge ni kuwafanya wananchi wake wafanye kazi kwa bidii na kuacha kushinda kwenye runinga wakiangalia bunge.

  Tayari Bunge limeshaelezwa sababu mbili tofauti za kukatisha matangazo hayo ambazo ni gharama ambazo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linalipia na hivyo kulazimika kupunguza matangazo hayo.

  Awali, Waziri wa Habari, Nape Nnauye ambaye alitoa tamko hilo bungeni, pia alisema vyombo binafsi vinaruhusiwa kurusha matangazo hayo moja kwa moja, lakini navyo vimepigwa marufuku.

  Sababu nyingine iliyotolewa na Nape ni kuwa uamuzi wa kuzuia matangazo hayo ulifanywa na Bunge la Kumi wakati likipitisha uamuzi wa chombo hicho wa kuanzisha studio yake.

  Lakini juzi, akiwa nchini Uingereza Majaliwa alikuwa na sababu nyingine ya kuzuia matangazo hayo kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.

  Akijibu swali kuhusu sakata hilo wakati akizungumza na Watanzania waishio London, Majaliwa, alisema kurusha moja kwa moja matangazo ya shughuli za Bunge ni kwenda kinyume na “Hapa Kazi Tu”, kaulimbiu ya Rais John Magufuli aliyoianzisha wakati wa kampeni.

  “(Kurusha shughuli za Bunge moja kwa moja) Maana yake ni kuwa katika kipindi cha Bunge la Bajeti ambalo linaendeshwa kila siku, Watanzania wangekuwa wanaangalia Bunge kwa miezi hiyo mitatu bila ya kufanya kazi,” alisema mtendaji huyo mkuu wa Serikali.

  “Tulilazimika kujifunza kutoka kwenye mabunge mengine. Hivi hapa Uingereza mnaangalia Bunge live kila siku?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa kuwa linarushwa moja kwa moja kwa kipindi kisichozidi dakika 15 wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu.

  Majaliwa alisema Bunge la Tanzania lilikuwa pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani ambalo lilikuwa likirushwa moja kwa moja kuanzia asubuhi hadi usiku.

  Waziri Mkuu aliendelea kufafanua kwamba Bunge la Tanzania linarusha moja kwa moja kila siku asubuhi wakati wa maswali ya kawaida na Alhamisi asubuhi wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu.

  Alisema mijadala yote hurekodiwa na kuhaririwa, kisha hurushwa kati ya saa 8:00 mchana na 9:00 alasiri na kati ya saa 3:00 na 4:00 usiku.

  “Kwa Watanzania wanaopenda kufanya kazi na wanaopenda kufuatilia mambo ya bungeni, walikuwa hawaoni ‘live coverage’ kwa sababu walikuwa kazini, lakini sasa hivi wanaweza kufuatilia masuala ya Bunge,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa muda wa jioni uliopangwa, mtu anakuwa ametoka kazini na anaweza kuangalia televisheni akiwa nyumbani.

  Source: Mwananchi

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku