• Breaking News

  May 15, 2016

  Mbaroni kwa kujiunganishia umeme kinyemela

   Shirika la ugavi wa umeme (Tanesco) Mkoa wa Pwani limemkamata mmoja wa wamiliki wa eneo la maegesho ya magari la White Star  Munira Mbowe kwa kosa la kujiunganishia umeme kinyemela.

  Mbowe ambaye ni mmiliki wa eneo hilo lililopo Kiluvya kwa Komba nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam alikamatwa jana baada ya kufanyika msako  wa kushtukiza kwa wateja mbalimbali  waliohisiwa kujiunganishia umeme.

  Mmiliki huyo wa Yadi  akiwa amejiunganishia umeme bila ya kufuata taratibu zozote za Tanesco ambapo ameisababishia shirika hasara ya zaidi ya sh. Mil. 50.

  Akizungumza kwenye Yadi hiyo ,Afisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Pwani Henry Byarugaba alisema baada ya kufanya ukaguzi waliweza kukuta mteja huyo akiendesha shughuli zake kwa kutumia umeme huo na kuisababishia Tanesco hasara ya Sh 50 milioni.

  "Tumekuwa tukibuni mbinu mpya kila kukicha ya kuwatia mbaroni wateja wetu wanaotuhujumu na leo ( jana) tumembana huyu anayedaiwa ni mmiliki wa Yadi ya White Star  baada ya kukuta anatumia umeme uliotokana na  kujiunganishia laini tatu za nyaya zinazopitisha umeme,” alisema Byarugaba

  Byarugaba alibainisha kuwa kwa sasa Mbowe amefikishwa kituo cha polisi Kibaha na utaratibu mwingine unaendelea.

  Alisema hii si mara ya kwanza kwa Mbowe kufanya hivyo  kwani walipofanya msako mwaka jana walimkuta amejiunganishia umeme na alichukuliwa hatua.

  Kwa upande wake Mbowe alijitetea kuwa hajui lolote kuhusu kuunganishiwa njia hizo tatu za umeme kwa sababu mara nyingi   hufanya shughuli zake jijini Dar es Salaam na shughuli zake nyingi pia huzifanyia huko jijini na ni mara chache huja hapo Kibamba.

  “Ni kweli tumekutwa na kosa na kuiba umeme lakini jamani nataka niwaeleze kuwa mimi sihusiki na kingine nawaomba msinitoe katika vyombo vya habari kwani haya ni maisha tu, sio vizuri kunitoa jamani mimi sihusiki kabisa katika wizi huu “ alijitetea Mbowe.

  Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Taneso Pwani Selemani Mgwila alisema kitendo alichokifanya mteja wao huyo ni kosa kubwa kwani umeme waliokuwa wanatumia katika ‘yadi’ ulisababisha upotevu wa makubwa.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku