• Breaking News

  May 14, 2016

  Mfumo Mpya wa CAF Utaipeleka Yanga Tena Ligi ya Mabingwa Msimu Ujao

  Na Baraka Mbolembole

  Taarifa kwamba kuanzia msimu ujao michuano ya klabu Afrika hatua ya makundi itakuwa ikianza kuchezwa na timu 16 bora si tu itafungua milango kwa klabu nyingi za Afrika Mashiriki na Kati kufuzu kwa wingi katika hatua hiyo, bali itafufua soka la Afrika kiujumla na ni wazi ushindani utakuwa mkubwa huku pia msisimko ukitaraji kuongezeka miongoni mwa mashabiki wa kandanda barani Afrika.

  Timu 16 ambazo zitagawanywa katika makundi manne yatakayokuwa na timu nnenne kila kundi zitakuwa na fursa nzuri ya kucheza michezo mingi ya kimataifa huku wakitaraji kupata mapato mengi kutokana na haki za matangazo ya televisheni, mahudhurio ya mashabiki uwanjani huku wachezaji wakitumia nafasi hiyo kukuza na kuonesha vipaji vyao zaidi na zaidi.

  CAF imeongeza mechi katika michuano hiyo huku timu zikiwa na nafasi kubwa ya kucheza game nyingi. Washindwa 16 wa hatua ya 32 wataangukia katika michuano ya Shirikisho wakati washindi 16 wao watafuzu kwa hatua ya makundi. Hii ni fursa zaidi kwa vilabu vinavyopata nafasi ya uwakilishi kutoka katika ligi kuu Tanzania Bara kujiimarisha ili kuweka mazoea ya kucheza kwanza katika hatua hiyo mpya.

  Simba SC, Azam FC kwa nyakati tofauti zimeweza kumudu kufika hatua ya 16 bora katika michuano ya Klabu bingwa au ile ya Shirikisho. Wakati Yanga ikiwa imefanikiwa kuwa miongoni mwa timu 16 katika michuano ya CAF mwaka 2015-kombe la Shirikisho, na mwaka huu katika klabu bingwa-walikotolewa na kuangukia katika michuano ya Shirikisho ni wazi nafasi hii itakuwa na maana zaidi kwa VPL.

  Ni vyema  Shirikisho la mpira nchini (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi nao wakaanza kujipanga ili kuwa na ligi bora zaidi ya ndani. Matatizo makubwa ambayo yanaukwamisha mpira wa miguu ni kuwapo kwa mfumo imara wa uzalishaji wa wachezaji vijana.

  TFF imeshindwa kusimamia sheria na kanuni za kuvitaka vilabu kuwa na timu za vijana. Vilabu vinakaidi hilo huku vikiwa na sababu ya msingi kwamba TFF yenyewe imeshindwa kuanzisha ligi imara ya vijana, kuanzia ngazi za madaraja ya chini. TFF inapaswa pia kusaka wadhamini ambao watawekeza katika ligi kuu ya vijana kama ilivyofanya Vodacom katika ligi.

  Kuimarisha nguvu ili kuziba mianya ya timu kupanga matokeo. Kuimarisha waamuzi ambao wamekuwa wakiharibu na kupoteza ubora wa ligi kutokana na uchezeshaji wao m-baya. Kuwa na ratiba yenye mpangilio mzuri kwa kufuata kalenda  ya FIFA, CAF na CECAFA ili kuondoa tatizo sugu la ligi kusimama kwa muda mrefu na kuharishwa mara kwa mara kwa michezo ya ligi.

  Kama tutakuwa na ligi bora yenye kutazamika bila shaka wawakilishi wetu CAF watajenga mazoea ya kufuzu katika hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa, na jambo hilo linaweza kufungua milango zaidi kwa Tanzania Bara kupata nyongeza ya nafasi katika uwakilishi wa klabu katika michuano ya CAF. Mabadiliko ya CAF yalete mabadiliko, ubora, ushindani katika VPL pia kuanzia msimu ujao.

  Ikiwa karibu kuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki kufuzu kwa hatua ya makundi katika michuano ya Shirikisho Afrika msimu huu, Yanga SC ambayo itakuwa Angola katikati ya wiki ijayo kulinda au kuongeza uongozi wao wa 2-0 dhidi ya Esperanca, ni wazi mfumo mpya wa CAF utawafanya mabingwa hao mara mbili mfululizo wa VPL kucheza tena hatua ya makundi ya michuano hiyo mwaka ujao.

  Mfumo mpya wa CAF utaipeleka tena Yanga ligi ya mabingwa msimu ujao. Yanga ilikuwa timu ya kwanza ya Afrika Mashariki kufuzu kwa hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa mwaka 1998.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku