• Breaking News

  May 22, 2016

  Mkuu wa Mkoa Aagiza Mkurugenzi, Mhazini Kukamatwa

  MKUU wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo ameagiza polisi mkoani humo kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Simon Mayeye na aliyekuwa Mweka Hazina, Emmanuel Joramu ili waweze kuhojiwa kuhusu ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za serikali.

  Mulongo ametoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha majumuhisho ya ziara yake aliyoifanya wilayani Bunda na kuagiza kuwa watuhumiwa wote wakabidhiwe kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG).

  Agizo hilo alilitoa kutokana na taarifa ya baraza la madiwani iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Issack Mayela inayohusu ubadhirifu huo wa mamilioni ya fedha ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 2.3, zikiwemo za ulipaji fidia wananchi wa kijiji cha Tairo ili kupisha eneo la uwekezaji (EPZ).

  Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa watumishi hao wa serikali ambao kwa sasa wamehamishiwa katika halmashauri nyingine watafutwe popote pale walipo na wakamatwe mara moja na kuhojiwa na kisha kutoa maelezo yao polisi, ikiwa ni pamoja na hatua za kinidhamu na za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

  “Huyo Mkurugenzi na Mweka Hazina ambao wametajwa katika taarifa hizo watafutwe mahali popote walipo na kisha kuhojiwa dhidi ya ubadhirifu huo na hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi yao…kazi hii naikabidhi CAG na Takukuru na waikamilishe ndani ya siku 14,” alisema

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku