• Breaking News

  May 8, 2016

  Mwarobaini Migogoro ya Ardhi Wapatikana..Hati Miliki za Kimila Kuanza Kutolewa

  Malinyi Baada ya kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika vijiji vingi hapa nchini, serikali kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi wameamua rasmi kutafuta mwarobaini wa kuondoa changamoto hiyo kwa kuanzisha mpango maalumu wa utoaji wa Hati Miliki za Kimila kwa kila ardhi ndani ya vijiji vyote nchini.

  Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa John Lupala amesema mpango huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi kupitia mafunzo watakayoyapata kupitia mradi wa kuanzisha programu kuwezesha Umilikishaji Ardhi(LTSP).

  Profesa Lupala alitoa kauli hiyo jana wilayani Malinyi dakika chache kabla ya kuanza kwa mkutano ulioshirikisha madiwani, maofisa ardhi, mipango miji, maofisa wa hifadhi na watendaji wa serikali kwa lengo la kuchambua na kuingiza maoni mapya katika rasimu ya kwanza ya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo.

  Hatua hiyo ni sehemu ya ziara ya siku nne ya watalaamu watakaotekeleza Hatimiliki za Kimila kwa wanakijiji zaidi ya 300,000 kwa wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi kupitia mradi huo.

  Kwa mujibu wa mradi huo wenye thamani ya dola 15.2milioni kupitia hisani ya nchi za Swideni, Denmark na Uingereza,umelenga ardhi na kugawa hatia hizo kuanzia mwaka huu hadi ukomo wake 2019.

  Alisema utekelezaji huo utategemea zaidi kushirikisha sekta binafsi. Alisema njia zinazotumika katika utekezaji wa mradi huo zitasaidia katika kurahisisha mpango wa miaka miaka kumi kwa vijiji vingine vyote nchini.

  “Kwa sasa nchi nzima ina vijiji takribani 12,000 na vijiji wastani wa 9000 vimeshapimwa mipaka yake lakini changamoto iliyopo ni kwamba, kuna vijijiji 1640 tu vilivyopangiwa matumizi ya ardhi, utaona bado safari ni ndefu,kwa hivyo mbali na mradi wa LTSP, kuna programu hiyo inakuja bado iko kwenye maandalizi,” alisema.

  Akizungumzia hali ya migogoro na hatua za utekelezaji wa mradi huo, Profesa Lupala alisema uwazi ndiyo utakaofanikisha kukamilisha ugawaji wa hati hizo na itakuwa fundisho kwa hatua nyingine za kusaidia wananchi ili ardhi wanayoitumia iwanufaishe kiuchumi.

  Kwa upande wake, Mwanasheria wa wilaya hiyo ya Malinyi, Beatrice Buya alisema asilimia 100 ya kesi anazopokea ofisini kwake ni migogoro ya ardhi. Alisema mbali na mradi huo wa LTSP, Julai  mwaka huu wilaya hiyo inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango mpya wa matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro.

  Isaya Mwilongo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Makelele, wilayani hapo alisema chanzo cha migogoro hiyo ni mchezo mchafu wa viongozi wa serikali za vijiji na kamati za ardhi kumilikisha ardhi kubwa kundi la watu wachache.

  “Mimi ni mmoja kati ya waathirika na leo nilikuja kuonana na wataalamu waniambie kwanini ardhi yangu ya kijiji cha Kihuvilile(hekari 4), sijapewa na mahamaka ya Ulanga na Kilombero zimeshaamua mwaka 2012 nikabidhiwe lakini kuna ujanja ujanja wa kutapeliwa kwa nguvu,”alisema.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku