• Breaking News

  May 9, 2016

  Taasisi ya Saratani Ocean Road ni Mateso

  Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imepewa asilimia 0.3 tu ya dawa ilizoomba wizarani kwa mwaka 2015/16, hali inayosababisha mateso kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

  Akizungumza na Mwananchi wiki iliyopita, Meneja Famasia wa ORCI, Albina Kirango alisema dawa hizo zimekuwa zikifikishwa hospitalini hapo kwa mafungu na kuanzia Julai hadi Septemba walipokea asilimia 0.02, Oktoba mpaka Desemba asilimia 0.05 huku Januari mpaka Machi wakipokea asilimia 0.2.

  Kirango alisema Ocean Road huagiza dawa kupitia Wizara ya Afya, kwa kuorodhesha idadi ya dawa wanazozihitaji na kuwasilisha Bohari Kuu ya Dawa (MSD), huku nakala nyingine ikipelekwa wizarani ambako hutolewa fedha kwa ajili ya kuzilipia.

  “Tunaweza kuagiza aina 15 za dawa za saratani, lakini iwapo wizara ikatoa kiasi kidogo cha fedha huletwa dawa zenye umuhimu, lakini za gharama ya chini ili angalau kuhudumia wagonjwa wengi zaidi, maana zipo dawa ambazo gharama yake ni Sh3 milioni mpaka 4 milioni kwa dozi ya wiki mbili,” alisema Kirango.

  Kiwango hicho cha dawa kilitolewa kulingana na kiasi cha fedha ambacho kimekuwa kikitolewa na Wizara ya Afya, kama bajeti ya matumizi ya taasisi hiyo inayohudumia zaidi ya wagonjwa 6,000 kila mwaka.

  Alisema dawa hizo za tiba ya saratani kwa kemikali ‘Chemotherapy’ zimekuwa zikiadimika zaidi hospitalini hapo, hivyo kuwafanya baadhi ya wagonjwa kulazimika kuzinunua nje ya hospitali katika maduka mbalimbali ya dawa.


  • “Katika dawa zote tunazoagiza, tumekuwa tukiletewa idadi pungufu, lakini dawa hizi zinapatikana kwa shida ukizingatia gharama zake kuwa kubwa,” alisema Kirango.


  Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipoulizwa alisema mbali na bajeti ya 2015/16, wizara ina mpango wa kuhakikisha tatizo hilo linatokomezwa na wagonjwa wanapata dawa.

  “Wizara kuanzia Januari mwaka huu wizara ilianza kutenga asilimia 13 ya bajeti ya dawa kila mwezi, kwa ajili ya dawa hizo na hadi sasa wizara imepeleka MSD Sh1.2 bilioni kwa ajili ya kununua dawa hizo na bohari hiyo inafanya utaratibu wa kuzinunua kwa wazalishaji hivyo tatizo hili litapungua,” alisema Ummy Mwalimu.

  Kwa mujibu wa Kirango, dawa ambazo zimekuwa zikipelekwa mara chache hospitalini hapo ni pamoja na Doxorubicine, Cyclophamide na 5FU ambazo hutibu saratani ya titi.

  “Kuna baadhi ya dawa kama ‘Cyclophamide’ tuna zaidi ya miaka minne hatujaletewa, Bevazicumas hii gharama yake ni Sh1.8 milioni, Rituximab Sh4.23 milioni, Transtuzuma Sh3.7 milioni na mgonjwa anatakiwa kupewa kila baada ya wiki mbili kwa kuwekewa kwa dozi sita,” alisema Kirango.

  Mkurugenzi wa Tiba wa Ocean Road, Dk Diwani Msemo alisema licha ya uhaba wa dawa hospitalini hapo, asilimia 80 ya wagonjwa wanaotibiwa hapo wanatumia tiba ya mionzi ambayo matibabu yake ni bure.

  Alisema tatizo ni kuwa baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakitumia dozi zote mbili yaani radiotherapy na chemotherapy kwa wakati mmoja, huku wengine wakitumia mojawapo kati ya hizo.

  “Tunashukuru bajeti mwaka huu imependekeza kutengwa kwa Sh9 bilioni kwa ajili ya dawa, hii itasaidia kwa wagonjwa ambao wanashindwa kumudu gharama, kwani wagonjwa pia wamekuwa wakiongezeka kila mwaka,” alisema Dk Msemo.

  Dk Msemo alisema wagonjwa wengi ni maskini, hivyo inakuwa vigumu kumudu matibabu na kusababisha wengine kurudi nyumbani kwa kukosa fedha kutokana na gharama iliyopo.

  “Matibabu ya saratani ni ghali, lakini Serikali ya Tanzania imekuwa ikitibia bure wakati mwingine mgonjwa anapofika anatakiwa kutibiwa kwa mionzi pekee, lakini tiba ya kemikali ni gharama,” alisema.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku