• Breaking News

  May 27, 2016

  Wauzaji Simu Feki Kurudisha Fedha au Kuwapa Simu Nyingine Wateja Wao

  Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imesema baadhi ya wafanyabiashara wako hatarini kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuuza simu bila leseni ikiwa waliouziwa simu feki watapeleka malalamiko baada ya kuzimwa Juni 16.

  Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alisema uuzaji wa vifaa vya mawasiliano bila ya kuwa na leseni ni kuvunja sheria.

  Mungy alisema ufungaji wa simu feki utasaidia kupunguza taka za kielektroniki ambazo ni hatari kwa mazingira na maisha ya binadamu.

  Wakati TCRA ikisema hayo, Tume ya Ushindani (FCC) imepigilia msumari kwa wafanyabiashara hao kupitia mwanasheria wake, Khadija Ngasongwa aliyesema wauzaji wanawajibika kwa wateja wao kwa kuwapa simu nyingine au kuwarudishia fedha.

  Katika semina kwa umma iliyofanyika Bukoba, pia Shirika la Viwango nchini (TBS) kupitia ofisa wake, Joyline Mwinuka liliungana na mamlaka hizo kuwatwisha mzigo wafanyabiashara hao ambao walizirushia lawama taasisi hizo kushindwa kudhibiti simu feki hadi kuingia nchini na wao kupata hasara.

  Pamoja na hayo, wafanyabiashara wa simu mkoani Kagera wameonyesha wasiwasi wa kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja ambao simu zao zitazimwa ifikapo tarehe hiyo.

  Mmoja wa wafanyabiashara hao kutoka wilayani Karagwe, Vicent Rushasi alisema wengi wao wamefilisika mitaji kwa kuathiriwa na uingizwaji wa simu hizo na vifaa vya magari.

  Wafanyabiashara Jamila Jamal na Rashid Katakweba walionyesha ugumu wa uwezekano wa kurudisha fedha au simu kwa wateja watakaolalamikia simu hizo wakisema inaweza kuleta mzozo.

  Kwa mujibu wa Mungy, hadi Machi mwaka huu kulikuwa na laini za simu 39.8 milioni nchini, idadi ya namba tambulishi ambazo hazikuwa na viwango zilikuwa asilimia nne na zilizokiliwa ni asilimia 13.


  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku