• Breaking News

  Jun 17, 2016

  Maandalizi ya CCM kumkabidhi JPM kijiti ndani ya saa 48

  Maandalizi ya CCM kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho ili ashike kofia zote mbili, yataanza kesho katika kikao cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

  Taarifa kuhusu kikao hicho iliyotiwa saini na msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ilisema: “Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM itafanya

  kikao cha kawaida siku ya Jumamosi jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kitafanyika chini ya mwenyekiti wa CCM Rais mstaafu Jakaya Kikwete.”

  Japokuwa taarifa hiyo haikueleza ajenda za kikao, habari kutoka ndani ya chama zinasema kikao hicho cha siku moja kinatarajiwa kujadili masuala mbalimbali, ukiwamo mchakato wa makabidhiano ya kiti hicho katika mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi ujao. Kipindi cha uongozi wa chama kwa Kikwete kitamalizika mwakani, lakini imekuwapo desturi kwa rais mpya kuachiwa kofia hiyo mapema, hivyo Rais Magufuli anatarajiwa kurithi mikoba ya uenyekiti mwezi ujao.

  Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelieleza gazeti hili kuwa kikao hicho kitajadili hali ya siasa nchini, muundo wa chama hicho na kupitia utendaji kazi wa Rais Magufuli huku Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana akikishauri chama hicho kubadili katiba yake ili Rais asiwe mwenyekiti wa chama.

  Vilevile, kikao hicho kinatarajiwa kuhitimisha hoja zinazodaiwa kuibuka katika vikao vya ndani vya chama hicho kwamba CCM inataka kuvuruga utaratibu uliodumu kwa muda mrefu wa mwenyekiti kumwachia kijiti Rais aliyeko madarakani.

  Madai kuhusu mkakati huo wa ndani yalisambazwa katika mitandao ya kijamii yakimnukuu Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, lakini Ole Sendeka alisema hana sababu yoyote ya kumjibu kiongozi wa dini.

  Februari 5, mwaka huu Kikwete alipokuwa anazungumza na wazee wa Manispaa ya Singida alisema sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya miaka 39 tangu chama hicho kuanzishwa zilikuwa za mwisho kwake akiwa mwenyekiti, kauli ambayo iliashiria ataachia mapema uenyekiti.

  Kwa desturi, wenyeviti wa CCM huwa wanaachia madaraka yao kabla ya muda wa uongozi wao kumalizika. Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikabidhiwa chama na Alhaji Ali Hassan Mwinyi mwaka 1996 badala ya 1997 na Mkapa alimkabidhi Kikwete kiti hicho mwaka 2006 badala ya 2007.

  Kulingana na kalenda ya chama hicho, Mkutano Mkuu wa CCM kumchagua mwenyekiti unapaswa kufanyika mwaka 2017, lakini utafanyika mwaka huu kuendeleza utamaduni wa kung’atuka mapema.

  Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kinachoendelea sasa mikoani na wilayani ni maandalizi ya mkutano huo mkuu yanayosimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti.

  “Kikao hicho cha Kamati Kuu ndicho kitakachojadili ajenda za mkutano huo sambamba na kupanga tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu,” zilieleza taarifa hizo.

  Dk Magufuli anatajwa kuwa uongozi wake ndani ya CCM utakuwa wa kasi ya aina yake kutokana na hatua mbalimbali za ‘utumbuaji majipu’ anazozifanya ndani ya Serikali tangu Novemba 5, alipoapishwa kuwa Rais.

  Maoni ya wachambuzi

  Akizungumzia kikao hicho, Dk Bana alisema kama angetakiwa kukishauri chama hicho, kauli yake ingekuwa moja tu ya kukitaka kuachana na utaratibu wa Rais kuwa mwenyekiti.

  Alisema Rais anatakiwa kuachwa afanye kazi yake ya kuongoza nchi na si kuvaa kofia nyingine ya kukiongoza chama na kutumia muda wa ziada kupambana na vyama vya upinzani.

  “Si lazima Kikwete aendelee na nafasi ya uenyekiti ingawa kafanya kazi nzuri. CCM ina watu wengi wazuri wanaoweza kushika nafasi hiyo na kukiongoza chama kwa mafanikio. Magufuli anapaswa kufanya kazi ya Serikali,” alisema Dk Bana.

  Kuhusu mambo yatakayojadiliwa, Dk Bana alisema chama hicho lazima kitaupitia upya muundo wake kutokana na kuwapo kwa miaka mingi, kiasi cha kuwa na idadi kubwa ya wajumbe, akitolea mfano wa Halmashauri Kuu aliodai hauna tija.

  “Lazima watajadili mwelekeo wa nchi kutokana na watu wengi kutoa kauli zinazoashiria kupingana na utawala wa Rais Magufuli hata katika masuala ya msingi kama kufuta sherehe, kutumbua majipu na kupandisha bajeti ya maendeleo mpaka asilimia 40,” alisema.

  Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu alisema: “Nadhani kitakuwa kikao kifupi sana na ajenda itakuwa kubadilishana uenyekiti tu.” “Wataepuka kujadili hali ya siasa nchini baada ya Uchaguzi Mkuu, utendaji kazi wa Rais Magufuli wala lile suala la utumbuaji majipu kama litahamia ndani ya chama chao.”

  Alibainisha kuwa mambo hayo hayawezi kujadiliwa kwa maelezo kuwa hayatakiacha kikao hicho salama.

  “Rais Magufuli aliwahi kutamka mbele ya Kikwete pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa amemwachia nchi ikiwa katika hali ngumu. Sidhani kama kuna mambo nyeti watazungumza katika kikao hicho,” alisema Profesa Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

  Alisema makada wa CCM hawawezi kusimama na kusema ukweli mbele ya Rais Magufuli kwa kuogopa kukumbana na ‘rungu’ lake na wangependa kufanya hivyo kupitia kivuli cha Kikwete ambaye anakabidhi kijiti

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku