• Breaking News

  Jun 18, 2016

  Marafiki wa Isaac, aliyekuhumiwa kwa kumtukana Rais, wamchangia mil 4.5 ya faini

  Marafiki wa Isaac Habakuk pamoja na wadau ambao hawakupendezwa na hukumu dhidi yake ya kwenda gerezani miaka 3 au kulipa faini ya milioni 7 kwa kudaiwa kumtukana Rais Magufuli kupitia mtandao wa Facebook kwa kutumia neno bwege wamemkabidhi jumla ya shilingi milioni 4.5 kwa ajili ya kulipa faini kuepuka kifungo gerezani.

  Akikabidhi fedha hizo Jijini Arusha mchana wa leo, mwakilishi wa marafiki hao, Ndg Ephata Nanyaro amesema fedha hizo zimekusanywa kutoka kwa marafiki mbalimbali ambao wametafutana kwa njia ya simu na kila mmoja kuchangia kuanzia sh 500 na kuendelea mpaka zikafika kiasi hicho.

  Fedha hizo ni makusanyo ya michango ya makundi mawili, moja likiratibiwa na Ephata Nanyaro na lingine likiratibiwa na Malisa Godilistern, wote wanachama wa Chadema na ambao hutumia mitandao ya kijamii kueleza mawazo yao kuhusu mambo mbalimbali.

  Nanyaro amesema wameamua kufanya harambee ya kumchangia kijana mwenzao aepukane na dhahama ya kutotumikia kifungo kwasababu kwa jinsi sheria ya makosa ya mtandao ilivyo, kila mwananchi yuko hatarini kupelekwa gerezani kwa sheria hiyo kwasababu inavifungu ambavyo vinakiuka msingi mkuu na uhuru wa binadamu kuwaza na kujieleza.

  Ameviasa vyombo vya Serikali vinavyosimamia sheria, hususani Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao kwa weledi huku wakisimamia sheria zinavyoelekeza tofauti na kitendo alichoeleza hakikustahili na sio haki kumuweka Isaac kizuizini kwa muda wa siku 28 bila dhamana wala kumfikisha Mahakamani kwa kosa ambalo halina kitisho cha hatari.

  Akifafanua zaidi, Nanyaro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Leveolosi ya Jijini Arusha amesema Isaac ataepuka kifungo kwa kulipa faini ya sh milioni 7 kwa awamu mbili ambao mpaka sasa amekwishakabidhiwa hizo milioni 4.5 na michango mingine inaendelea huku ahadi zikivuka kiwango hicho.

  Nae Isaac alipopewa fursa ya kuzungumza amewashukuru sana watu wote ambao wamejitolea kumchangia na kueleza kuwa wameonesha upendo wa kipekee na moyo wa ajabu katika kadhia inayomkabili. Amewasihi kuendelea na moyo huo kwa kusaidia na wengine wanapokuwa na uhitaji.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku