• Breaking News

  Jun 17, 2016

  Mtoto wa Miaka 9 Aichambua SMG Mbele ya Kamanda Sirro

  Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuna vikundi vinavyowapeleka watoto porini na kuwapa mafunzo ya kigaidi.

  Alisema jeshi hilo liliwahi kumkamata mtoto wa miaka tisa, katika pori lililopo wilayani Mkuranga, Pwani, aliyepewa mafunzo ya kigaidi na kuwastaajabisha kwa kuwa na uwezo wa kuichambua silaha ya kivita.

  Sirro aliyazungumza hayo jana wakati wa ibada ya shukrani iliyofanyika katika Kanisa la Katoliki Parokia ya Makabe Bikira Maria, katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

  Aliwataka viongozi wa Serikali za mitaa kutoa ushirikiano, pindi wanaposikia mzazi amemuachisha mtoto shule na kumpeleka porini kwa ajili ya mafunzo ya kigaidi.

  “Haya mambo yanafanyika kwenye mitaa yetu, lakini kinachojitokeza kiongozi wa Serikali ya mtaa anaposikia kuna mtoto wa fulani amejiunga kwenye vikundi viovu, hawatoi ushirikiano kwa Jeshi la Polisi,” alisema.

  Akiwa katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha watoto wanaoishi mazingira magumu cha Child in the Sun, Sirro alisema kuna kikundi kimeibuka ambacho kinawachukua watoto wa shule na kuwapeleka porini, kwa ajili ya mafunzo hayo ambayo alisema hayajengi nchi bali yanabomoa.

  Padri wa Parokia hiyo, John Maendeleo aliishauri jamii kuwajengea mazingira mazuri watoto wao ili waweze kuepukana na vitendo vya kihalifu.

  Padri Maendeleo aliwataka wazazi wawajibike kwa watoto wao ili wasiingie kwenye dhambi ya uvivu, kwa kumuweka mbele Mungu kwani watakuwa kwenye maadili mema.

  Wakati huo huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema kutofanyiwa marekebisho kwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971, inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 15, bado ni tatizo nchini.

  Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Francis Nzuki alisema kutoondolewa kwa kipengele hicho ni changamoto, ingawa tatizo hilo linatatuliwa kwa mtoto kupelekwa shule. “Sheria ya elimu inatatua changamoto hiyo ya kisheria, kwa yeyote atakayekatisha masomo ya mtoto kwa namna yoyote kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

  Alisema adhabu ya miaka 30 kwa atakayekatisha masomo au kifungo cha maisha, imesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa changamoto za ukandamizwaji wa haki za mtoto ikiwa ni pamoja na kukosa nafasi ya kupata elimu.

  Alisema kuongezeka kwa vitendo vya kikatili katika jamii kunasababishwa na kukosekana kwa elimu na umaskini katika jamii.

  Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la World Vision, John Massenza alisema kumekuwa na vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto huku jamii ikiwa kimya.

  Alisema Shirika la World Vision limekuwa mstari wa mbele kupigania haki za watoto, lakini wamekuwa wakipata vikwazo kutoka kwenye jamii kufichua maovu yanayotokea, hivyo kuihimiza kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika.

  Imeandikwa na Pamela Chilongola, Colnely Joseph na Filbert Rweyemamu.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku