• Breaking News

  Jun 5, 2016

  Prof. Mwandosya Atoa Ufafanuzi Juu ya Elimu yake

  Mwaka 1967 Serikali, kupitia Wizara ya Elimu ya Taifa ilianzisha sera ya kuwa na shule ambazo zingechukua wanafunzi wenye vipaji, waliofanya vizuri na kupata alama za juu kwenye masomo ya sayansi na hisabati katika mitihani ya kidato cha nne.

  Katika mfumo huo taasisi/shule mbili, Chuo cha Ufundi Dar es Salaam, na Sekondari ya Kibaha, zilichaguliwa kudahili wanafunzi waliopata alama za juu katika hisabati, fizikia, na kemia, kuchukua masomo ya Hisabati, Hisabati, na Fizikia (Pure Mathematics, Applied Mathematics, and Physics) kidato cha tano na cha sita(Advanced Level au A-Level).

  Chuo cha Ufundi Dar es Salaam kilichaguliwa kuanzisha masomo ya kidato cha tano na cha sita mbali na mafunzo ya kawaida ya cheti(Full Technician Certificate). Kozi hizi mbili zilienda sambamba lakini zilikuwa tofauti. Masomo ya kidato cha tano na sita yalilenga katika kuwatayarisha wanafunzi ambao baada ya kumaliza na kufaulu wangeenda vyuo vikuu kusomea uhandisi.

  Mbali na mchepuo wa Hisabati, Hisabati na Fizikia, wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita Chuo cha Ufundi Dae es Salaam walichukua masomo ya ziada ya Uchoraji katika Uhandisi (Engineering Drawing) na mazoezi ya karakana (Workshop Practice).

  Masomo haya yalitolewa katika azma ile ile ya kuwatayarisha wanafunzi kuchukua uhandisi vyuo vikuu lakini hawakutahiniwa katika masomo haya ya ziada. Mchepuo huu ulianza mwaka 1968 na pamoja na mafanikio makubwa ulihitimishwa mwaka 1972.

  Baadhi ya wanafunzi waliopitia mchepuo huo ni Profesa Mathew Luhanga, Profesa Lunogelo Mwamila, Profesa Mark Mwandosya, Eric Mugurusi, Majani(RIP), Profesa Maurice Mbago, Kassim Mpenda, na wahandisi na wataalamu wengi mashuhuri.

  Kwa kumalizia, si kweli kwamba Profesa Mwandosya alipata cheti cha ufundi halafu akaenda Chuo Kikuu cha Aston Uingereza, bali alipata alama za juu kidato cha sita katika mchepuo wa Hisabati, Hisabati, na Fizikia (Pure Mathematics, Applied Mathematics, and Physics), msingi uliomwezesha hatimaye kupata shahada ya uhandisi umeme daraja la kwanza( First Class Honours), Chuo Kikuu cha Aston, Uingereza, na hivyo kuruhusiwa kufanya shahada ya uzamifu (PhD), Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza, moja kwa moja bila kupitia shahada ya uzamili(Masters).

  Rafiki yangu yeyote wa fb anayemfahamu Ndugu Malisa GJ,mwandishi na mchangiaji wa makala katika mitandao ya kijamii, tafadhali mpatie taarifa hii. Shukrani.

  Mark Mwandosya.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku