• Breaking News

  Jun 17, 2016

  Profesa Ibrahim Lipumba Akoroga Wanachama

  MWENYEKITI wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu, amewagawa wanachama wa vyama vya siasa mkoani Tabora kutokana na kauli ya kutaka kurejea kwenye nafasi hiyo.

  Wakizungumza na gazeti hili, walisema wao wamamheshimu Profesa Lipumba kwa mchango wake lakini akumbuke aliwaacha kipindi kigumu cha uchaguzi Oktoba, 2015, hivyo kuhoji anarejea kutafuta nini.

  Kiongozi mmoja wa ngazi ya wilaya wa CUF alikuwa tofauti kidogo na wenzake kwa kusema ni kosa kutamka Lipumba alijiuzulu wakati ukisoma Katiba haisemi hivyo. Huku akikataa jina lake lisiandikwe gazetini, alisema alichofanya kilikuwa sahihi kwa kipindi kile kwani alipuuzwa.

  Bwiru Maulid ambaye ni mwanachama wa ACT-Wazalendo alisema licha ya kuwa siyo mwanachama wa CUF, lakini alidai kuwa mchumi huyo mbobezi anashauriwa vibaya na baadhi ya watu. Alisema pamoja na kwamba haijui Katiba ya CUF lakini bado anashangazwa na kile ambacho kilimfanya ang’atuke kwani bado vilivyomwondoa vipo hadi sasa.

  Alisema anaona kama Profesa Lipumba anaenda kufanya fujo na kutaka kukigawa chama chake. Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kaliua, Lubaga Katwiga alikuwa tofauti na wenzake, akieleza kuwa alichoamua Profesa Lipumba ni sahihi kwani ametengua barua ya kujiuzulu kwake.

  Katwiga alisema chama chao kwa muda kilikuwa hakina msemaji mkuu hivyo anaona siku ya uchaguzi wanakwenda kumrejesha mwenyekiti wao Lipumba. Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Francis Msuka alisema inashangaza zaidi kwani wakati wakiwa kwenye uchaguzi, Lipumba alijiuzulu kwa mbwembwe.

  Alisema kwa dhana ya kugawana majimbo kabla ya Profesa Lipumba hajajiuzulu, wangetwaa majimbo mengi, akitolea mfano wa Jimbo la Tabora Mjini, Jimbo la Sikonge na viti kadhaa vya udiwani ikiwamo Kata ya Ilolangulu, mahali alipozaliwa profesa huyo wa uchumi miaka 64 iliyopita.

  Alisema kurejea kwa Lipumba anaona kama inakuja shida na pengine shida hiyo ikahamia hata vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini hata hivyo anawaachia CUF wenyewe.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku