• Breaking News

  Jun 28, 2016

  Wakuu wa Wilaya Wapya, Muwe Tochi ya Maendeleo

  KWANZA nianze kumuomba Mungu azidi kutupa afya njema ili tuweze kumtumikia vema na kutumikia taifa letu huku tukidumisha amani yetu.

  Leo nizungumze na wakuu wa wilaya wapya walioteuliwa na Rais Dk. John Pombe Peter Magufuli juzi Jumapili ambao hakika ndiyo viongozi walio karibu zaidi na wananchi wa chini kabisa. Nasema hivyo kwa sababu mkuu wa wilaya ndiye anayeshughulika na serikali za vijiji au mitaa moja kwa moja na ndiye anayekutana mara nyingi na wananchi hao kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo katika ngazi hizo za chini za uongozi.

  Bila shaka watajulishwa majukumu yao lakini ni wazi kwamba watatakiwa wasishinde ofisini badala yake wawe kwenye vijiji au mitaa kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi.
  Mkuu wa wilaya ndiye mwakilishi wa rais katika ngazi ya wilaya na ndiye ana majukumu ya kuhakikisha usalama katika wilaya yake ndiyo maana anakuwa moja kwa moja mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya.

  Ni jukumu la kila mkuu wa wilaya kuhakikisha wilaya yake haina wavurugaji wa amani ambao ni pamoja na majambazi na watu wanaoua watu kwa njia mbalimbali.
  Niwaambie ukweli wakuu wa wilaya wapya kwamba ili mfanikiwe ni lazima muwe karibu na wananchi wa kawaida kwa sababu hao ndiyo wanaokaa na watu, wawe wema au wabaya.
  Kila mkuu wa wilaya ni lazima awe pia karibu na wana habari kwa sababu hao hujikita zaidi na wananchi mitaani ndiyo maana wanapata habari wakati mwingine nyeti za kusaidia amani na utulivu nchini.

  Niwasihi wakuu wa wilaya kuepuka ushabiki wa kisiasa. Wapo ambao wanapendelea mara kwa mara kujikita katika siasa wakati wanajua wao wanahudumia watu wa vyama vyote. Mkuu wa wilaya kujiingiza katika siasa za moja kwa moja ni kosa kwa sababu watu wa upande wa pili wanaweza kuwatenga.

  Nasema hivyo kwa sababu kuna wilaya zimekamatwa na wapinzani kwa maana ya halmashauri ya wilaya inaongozwa na wenyeviti wapinzani ni jukumu la mkuu wa wilaya kufanya kazi vizuri ili wilaya hizo nazo zipate maendeleo kwa sababu wanaohudumiwa siyo vyama bali ni wananchi.
  Nasema ni wananchi kwa sababu upo ushahidi kwamba katika wilaya nyingine kuna wananchi ambao siyo wanachama wa vyama vya siasa ndiyo maana katika katiba pendekezwa ikapendekezwa kuwa wasio wanachama wa vyama vya siasa nao waruhusiwe kupigiwa kura.

  Kwa maana hiyo niwasihi wakuu wa wilaya wapya kuacha kuegemea chama licha ya kujua kwamba wameteuliwa na kiongozi ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi.
  Maana yangu ni kwamba shughuli za chama zisihusishe moja kwa moja na shughuli za maendeleo kwa kuwa kwa kufanya hivyo, mtapoteza watu wa upande wa pili hivyo kukosa kile kilichokusudiwa.

  Mwisho, nimpongeze Rais Dk. Magufuli kwa hatua yake ya kuchagua vijana wasomi kutuongozea wilaya zetu tukiwa na imani kuwa watachapa kazi kama alivyoonesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye haraka haraka amepanda na kuwa mkuu wa mkoa kutoka wilayani. Huyu anaweza kuwa tochi yenu nanyi mkawa tochi ya wananchi. Atakayekwenda kwa kuchechemea, ataachwa nyuma!

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku