• Breaking News

  Jul 26, 2016

  Mbunge amtembelea mwenye risasi miaka 8

  Katika hali inayoonesha kuwa ameguswa na unyama aliotendewa Hassani Athumani (30), mkazi wa Kiabakari, wilayani Butiama, Mara anayeishi na risasi mwilini kwa miaka nane, Mbunge wa Viti Maalum mkoani Mara, Joyce Sokombi (Chadema) alilazimika kumwaga machozi hadharani baada ya kumtembelea nyumbani kwao na kumshuhudia anavyoteseka.

   Mbunge wa Viti Maalum mkoani Mara, Joyce Sokombi (Chadema) akiongea na Hassani alipomtembelea nyumbani kwao Kiabakari.

  Mbunge huyo (pichani) alifika kumuona mgonjwa huyo ambaye habari zake ziliandikwa na gazeti hili katika toleo lake la Julai 5-11,2016 na alishuhudia jinsi anavyoteseka huku mwili wake ukiwa umejaa vidonda na kupooza.

  Aidha, Sokombi baada ya kumwona mgonjwa huyo aliyepooza kutokana na kupigwa risasi Machi 6, 2008 na majambazi, alitoa mchango wa shilingi 200,000 kwa ajili ya kumsaidia.


  “Natoa wito kwa Watanzania wengine wakiwemo wanasiasa hususan Mbunge wa Jimbo la Butiama, Nimrod Mkono kumsaidia mgonjwa huyo anayehitaji fedha za matibabu, chakula na mavazi,” alisema mbunge huyo huku akitokwa machozi.

  Mbali na mbunge huyo, wajumbe wa Chadema wa Kanda ya Serengeti wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Kukirango, Issa Khazi nao walimtembelea mgonjwa huyo.

   “Tunawapongeza sana Uwazi kwa ufuatiliaji wao wa habari za kijamii na hatimaye kuibua habari ya mgonjwa huyu, tunaviomba vyombo vingine vya habari kuiga mfano wa Global,” alisema diwani huyo.

  Global Publisher

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku