• Breaking News

  Jul 30, 2016

  Mwandishi wa Nipashe Afungwa Jela Kwa Kuiba TV

  MAHAKAMA ya Mwanzo ya Usambara mjini Tanga imemhukumu kifungo cha miezi sita nje mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe, Dege Masoli kwa wizi wa televisheni moja ya kisasa aina ya Samsung flat screen inchi 32 pamoja na kompyuta moja mali ya Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Tanga (TPC).

  Imemwamuru pia kulipa fedha taslimu Sh milioni 1.8 kabla ya kumaliza kifungo hicho cha miezi sita ili kufidia gharama ya vifaa hivyo alivyoiba. Akisoma hukumu hiyo Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Usambara, Agnes Sehoza alisema mahakama imejiridhisha bila kutia shaka kwamba mlalamikiwa Masoli alitenda kosa hilo.

  “Kulingana na maelezo yaliyotolewa na mlalamikaji ambaye ni Mwenyekiti wa TPC Hassan Hashim, shahidi mmoja kati ya tisa waliopangwa kusikilizwa pamoja na vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa hapa… mahakama hii imeridhika na inakutia hatiani kwa fungu namba 32, kifungu kidogo cha kwanza, kifungu cha tatu cha Sheria ya Makaosa ya Jinai ya mwaka 2004,” alisema na kuongeza: “Kutokana na utetezi wako ambao umeuwasilisha mbele ya mahakama hii kwamba awali hukuwahi kutenda kosa kama hili, una familia kubwa inayokutegemea yenye wake wawili pamoja na watoto wanane, mahakama hii imeamua utumikie kifungo hicho nje ili kunusuru ustawi wa familia, lakini utalazimika kulipa fedha hizo kabla ya kumaliza adhabu yako na katika kipindi hicho hutakiwi kufanya kosa lolote la jinai,” alisema.

  Awali ilidaiwa mahakamani hapo kwamba Januari 17 mwaka huu kati ya saa 1:00 hadi saa 5:00 asubuhi mlalamikiwa Masoli alichukua funguo za ofisi ya TPC kutoka kwa Mratibu wao, Neema Hatibu kwa lengo la kuingia ofisini na ndipo alipotenda kosa hilo.

  Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba siku hiyo ya tukio Mratibu wa TPC alimuamini mlalamikiwa na kumkabidhi funguo hizo za ofisi kwa kuwa kiutendaji Masoli alikuwa ndiye Katibu Msaidizi wa Klabu.

  Hivyo aliomba atangulie kuingia ili atumie kompyuta kutuma habari na pia alidai angetumia muda huo kuwasubiri viongozi wenzake wengine ili kushiriki nao kikao cha kuandaa mpango mkakati wa klabu yao ambacho kilitarajiwa kufanyika baadaye mchana.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku