• Breaking News

  Aug 13, 2016

  Agizo la JPM Lawavuruga Profesa Muhongo, Wabunge

  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo juzi aliwashukia wanasiasa wa Mkoa wa Geita kwa kumchongea yeye na viongozi wa mkoa kwa Rais John Magufuli ili waonekane hawatekelezi agizo la kuwagawia wananchi magwangala.

  Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara mjini Kahama mwishoni mwa Julai, Rais aliagiza viongozi wa mkoa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) waandae utaratibu wa kuwagawia wananchi magwangala ili yawasaidie kuendesha maisha yao.

  Rais alipiga marufuku kuwanyima wananchi udongo huo wenye masalia ya dhahabu ambao humwagwa na mgodi wa GGM kwa kuwa wamiliki wa mgodi walikuja kutafuta dhahabu na si magwangala.

  Juzi, akitangaza utaratibu wa kuanza kugawa magwangala hayo, Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuwasema wanasiasa wa Mkoa wa Geita kwa kutokuwa na subira na badala yake kwenda kwa Rais kuwachongea ili viongozi wa mkoa na wizara waonekane hawafanyi kazi.

  “Wanasiasa tuliwaeleza wazi kwamba kwa kushirikiana na Nemc tunatafuta maeneo ambayo ni rafiki na hayana madhara ya kimazingira, lakini nyinyi wanasiasa mkapeleka kilio kwa Rais mara ya tatu mkidai mpewe magwangala,” alisema Profesa Muhongo.

  “Mmekosa uvumilivu. Tulisema mvumilie tukague na tuone hakuna madhara, lakini hamkukubali. Tunakubaliana hapa baadaye nyie mnaenda kudai kwa Rais wakati huku kuna zebaki yenye madhara makubwa. Lakini kutokana na nyie kutokuwa wavumilivu, ndio imesababisha haya yote.”

  Profesa Muhongo alitangaza kuwa magwangala hayo yangeanza kutolewa juzi saa tisa alasiri ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais la kugawa udongo huo ndani ya wiki tatu.

  Aliyataja maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kumwaga magwangala kuwa ni Nyamikoma, Lwenge, Kasota na Samina B.

  Akizungumzia lawama hizo, Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu alisema wabunge walilazimika kumweleza Rais suala hilo kutokana na muda mrefu kupita bila ya ahadi hiyo kutekelezwa.

  Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alipingana na uamuzi wa Serikali wa kutumia eneo moja ambalo pembeni kuna chanzo cha maji.

  Peneza alionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa waziri kukubali matamko ya wanasiasa na kuridhia wananchi kugawiwa magwangala pembezoni mwa chanzo cha maji akisema Profesa Muhongo ni msomi anayejua madhara ya kemikali zinazotumika kuchenjua dhahabu.

  Kauli ya Peneza ilipokelewa kwa hisia tofauti na wabunge wenzake pamoja na mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambaye alisema hatua iliyofikiwa sasa imetokana na utekelezaji ambao wanasiasa waliutaka.

  Waziri Muhongo alikiri kuwa kemikali ya zebaki ni hatari na kutoa mfano wa maeneo ya Mpanda ambako utafiti unaonyesha wananchi wana sumu ya zebaki mwilini.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku