• Breaking News

  Aug 18, 2016

  Askofu Aelezea Hofu Ushoga Kupandikizwa

  ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Same, Rogatus Kimario amesema ipo mikakati kupitia mitandao ya kijamii kuingiza ndoa za jinsia moja nchini na kusisitiza ikiwa watu wenye kumwamini Mungu hawataweka mikakati katika hilo, zitaingia.

  Aliyasema hayo jana alipokuwa akihubiri katika Kongamano la Jubilee ya miaka 35 ya Karismatiki Katoliki Tanzania.

  Karismatiki ni moja ya chama cha Kitume katika kanisa hilo. Alisema Wakristo na watu wenye kumwamini Mungu kama hawataweka mikakati ya kupambana na uovu na uvunjifu wa maadili, itakuwa hatari katika jamii.

  “Dunia nzima kuna watu wanafanya wanavyotaka. Kama upo katika ‘Whatsapp’ na Facebook kuna vikundi vimejipanga kuingiza ndoa za jinsia moja Tanzania, wapo kimkakati kabisa, tusipoangalia wataingia,” alisema Askofu Kimario.

  Akisisitiza kuhusu Wakristo kujipanga kimkakati, alisema lazima kuruhusu neno la Mungu lihubiriwe sana kwa watu wote na kusimamia ukweli.

  Alisema uhuru wa dunia kutumia mitandao ya kijamii katika kutekeleza mambo yao unapaswa kuhamia kwa wanaomwamini Mungu ili kuzuia maovu katika jamii.

  Akizungumzia Jubilee hiyo ya miaka 35 ya Karismatiki, alisema ni neema za Mungu kufika miaka hiyo na kuwaagiza Wakarismatiki na Wakristo wote kuliishi Neno la Mungu na kutokuwa wavivu kusoma na kuliishi.

  Kuhusu Karismatiki, alisema wapo watu wanaweza kudhani imechelewa kuanza ndani ya kanisa, lakini wanapaswa kutambua kuwa wakati wa Mungu ndio sasa na kutakiwa kuruhusu Roho Mtakatifu awatumie.

  Juzi akifungua kongamano hilo la Jubilee ya Karismatiki Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya alimshukuru Mungu na kuwapongeza Wakarismatiki kwa miaka hiyo 35 kuwapo ndani ya kanisa. Aliwataka kuiombea Serikali katika hatua yake ya kuhamia Dodoma na kusisitiza hatua hiyo ni neema kwa Dodoma.

  Alisema kongamano hilo limefanyika Dodoma ikiwa ni mpango wa Mungu na kusisitiza kuwa Serikali inatakiwa kuombewa ili lengo hilo litimie na Mungu atukuzwe.

  Kuhusu, Kongamano hilo Askofu Mkuu Kinyaiya alisema, katika kumshukuru Mungu Wakarismatiki wanapaswa kumuomba Mungu sana.

  Amewataka kumuomba Mungu awape nguvu za kuwaendea wahitaji na ambao hawajaonja neema za Mungu ili wazipate.

  Aliwahamasisha wakristo kuacha kulewa pombe na badala yake walewe Roho Mtakatifu maana katika yeye amani, furaha na upendo vinapatikana. Karismatiki Katoliki ni chama cha Kitumendani ya Kanisa kilichoanza nchini mwaka 1981 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris Jimbo la Morogoro kikiwa na idadi ya watu 23 wakiwamo mapadri.

  Hivi sasa kimeenea katika majimbo yote nchini. Zaidi ya watu 3,000 wanashiriki kongamano hilo kutoka majimbo yote ya kanisa hilo nchini, nje ya nchi wamo kutoka Marekani, Roma, Canada, Uganda na Kenya, Askofu wa Tanga, Anthony Banzi alikuwepo pia.

  Miongoni mwa wageni wanaoshiriki kongamano hilo lililoanza Agosti 16 hadi Agosti 21 ni pamoja na Rais wa Karismatiki kutoka Ofisi ya Baba Mtakatifu, Michelle Moran ambaye anahubiri, wahubiri wengine ni kutoka ndani na nje ya nchi na waumini walei.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku