• Breaking News

  Aug 18, 2016

  Azam Yafuta Uteja Kwa Yanga, Yatwaa Ngao ya Jamii

  Azam FC imefuta uteja kwa Yanga katika michezo ya kuwania Ngao ya Jamii baada ya leo kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penati 4 kwa 1, katika dimba la Taifa Dar es salaam, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 2-2.

  Kikosi cha azam pamoja na viongozi wao, baada ya kutwa Ngao ya Jamii
  Mechi hiyo ambayo ni maalum kwa ajili ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umezikutanisha timu hizo mbili kwa msimu wa 4 mfululizo ambapo Yanga imekuwa ikiinyanyasa Azam kwa kutwaa gao hiyo katika miaka yote mitatu iliyopita.

  Katika Mchezo wa leo, Yanga ambao waliingia uwanjani kwa kujiamini zaidi kuliko Azam walionesha Kandanda safi katika dakika zote 45 za Kwanza, na kutawala mchezo kwa kandanda safi kupitia kwa nyota wake, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, huku ukuta wake ukilindwa vilivyo na raia wa Togo, Vincent Bosou.

  Alikuwa ni raia wa Zimbabwe Donald Ngoma aliyepeleka chereko Jangwani kwa kuandika bao la Kwanza kufuatia shambulizi kali lililofanywa na Yanga waliokuwa wakicheza kwa 'kasi ya kimataifa' ikiwa ni dakika ya 20 na dakika 2 baadaye dakika ya 22, Ngoma huyohuyo akapachika bao la pili kwa mkwaju wa penati.

  Mashabiki wa Yanga walikuwa wakishangilia kwa muda wote hadi dakika ya 74 pale ambapo Shomari Kapombe alipunguza shangwe zao baada ya kuipatia Azam bao la kwanza, hali iliyoilazimu Yanga wabadilike na kuanza kucheza mchezo wa kujilinda zaidi.

  Azam waliendeleza mashambulizi ya hapa na pale yaliyowazawadia penati katika dakika ya 89, na penati hiyo kufungwa na nahodha John Bocco, na kufanya matokeo kuwa sare ya 2-2 hadi dakika 90 zilizpo kamilika.

  Katika hatua ya mikwaju ya Penati, wachezaji wa Yanga Hassan Ramadhan Kessy na Haruna Niyonzima walikosa penati zao huku golikipa Deo Munisi Dida ambaye ndiye aliyepiga penati ya kwanza kwa Yanga akifunga penati yake.

  Azam iliyopiga penati nne, wapigaji wake John Bocco, Himid Mao, Shomari Kapombe na Kipre Balou wote walitikisa nyavu na kufanya matokeo kuwa 4-1.

  Kumalizika kwa mechi hiyo ni mwanzo wa msimu mpya wa ligi kuu Tanzania, wakati Yanga ikijiandaa kuelekea nchini DRC kuikabili TP Mazembe katika mchezo wa kukamilisha ratiba wa kombe la Shirikisho Afrika, Kundi A.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku