• Breaking News

  Aug 9, 2016

  Bavicha Watoa Neno...Kamwe Hatutashiriki Kumjaribu Rais John Magufuli

  BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limesema kamwe wanachama wake hawatashiriki kumjaribu Rais John Magufuli, bali watasaidia kuonesha upungufu ndani ya serikali.

  Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi wakati akitoa tamko la kuunga mkono azimio la Baraza Kuu la Chadema juu ya kufanya maandamano nchi nzima Septemba Mosi, mwaka huu.

  Katambi alisema katika kuhakikisha kuwa hawamjaribu Rais Magufuli kama ambavyo Rais alitahadharisha hivi karibu, watafuata taratibu zote kisheria kuomba vibali vya kufanya mikutano hiyo.

  “Hatutaki kumjaribu Rais na haya tunayoyafanya ni katika kuunga mkono utekelezaji wa majukumu yake kwa kumuonesha upungufu katika serikali, ”alisema Katambi.

  Alisema katika kuendesha shughuli zao za siasa na kwa kuhakikisha kuwa mikutano ya Septemba Mosi mwaka huu inafanyika nchi nzima, chama hicho kitahakikisha kinafuata taratibu zote za kisheria zinazoviongoza vyama vya siasa ili kuruhusiwa kufanya mikutano na maandamano.

  Alisema kuwa maandalizi ya maandamano hayo pamoja na mikutano yanaendelea vyema nchini kote na yataenda sambamba na kupinga vitembo mbalimbali vya unyanyasaji unaofanywa kwa wanasiasa wa upinzani.

  Katambi alisema endapo chama hicho kitanyimwa fursa ya kuendesha shughuli zake za kisiasa nchini kwa kuanzia na mikutano yao ya Septemba Mosi watatoa uamuzi wa njia stahiki za kuidai haki hiyo baada ya hapo.

  Alisema Bavicha itaendelea na maandalizi na itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha masuala yote muhimu yanayoendelea hapa nchini yanasemwa hadharani mahali popote na kwa gharama yoyote.

  Kamati Kuu ya dharura ya Chadema iliketi kuanzia Julai 23- 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kuazimia kuwa Septemba Mosi, mwaka huu ni siku ya mikutano ya hadhara nchi nzima.

  Kamati hiyo iliagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya Msingi, Kata, Majimbo, Wilaya, Mikoa, Kanda, Mabaraza na Taifa kukaa vikao vyake vya kikatiba na kuvielekeza ajenda ya vikao hivyo kuwa ni kujadili hali ya siasa, hali ya uchumi na maandalizi ya mikutano hiyo.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku