• Breaking News

  Aug 1, 2016

  Edward Lowassa Aibukia Klabu ya Simba

  EDWARD Lowassa jana aliibukia kwenye Mkutano Mkuu wa Simba, hakufika kwa umbo lakini staili yake ilifika. Unaikumbuka ile staili ya ushangiliaji iliyokuwa inatumiwa na mgombea huyo wa urais katika uchaguzi uliopita kupitia Chadema kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)? Basi aina yake ya ushangiliaji iliteka mkutano huo.

  Simba walifanya mkutano wao huo jana kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Masaki jijini Dar es Salaam uliohudhuriwa na wanachama 700.
  Katika mkutano huo uliokuwa wa vituko na vioja vingi kutoka kwa wanachama hao, walikubaliana kupitisha ajenda kumi ambazo zote zilipitishwa chini ya Rais, Evans Aveva.


  Lakini kabla hata mkutano haujaanza watu walionekana wanataka mabadiliko. Mkutano huo ulianza saa 5:08 asubuhi huku baadhi ya wanachama wakionekana kutaka mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa timu hiyo.

  Dalili hizo za wanachama hao kutaka mabadiliko zilianza mapema kabla ya rais wa timu hiyo kuanza kupitia ajenda pale alipotoa salamu kwa kutamka Simba na wenyewe wanachama wakatamka mabadilikoo, huku wakiichezesha mikono yao kama ile staili ya mabadiliko iliyoanzishwa na Ukawa baada ya kumpata Lowassa.

  Lowassa alivuma sana kwa staili hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba, mwaka jana. Lilipokuwa likitamkwa jina lake Lowassaaaa, watu waliitikia mabadilikooo, ilipotamkwa mabadilikooo, waliitikia Lowassaaa. Sasa jana ilikuwa ni “Simbaaa” halafu watu wanaitikia mabadilikooo.”

  Kimsingi, wanachama karibu wote waliohudhuria mkutano huo wa jana, walitaka timu hiyo apewe Mohammed Dewji, maarufu kwa jina la Mo ambaye anataka kununua hisa asilimia 51 za klabu hiyo kwa dau la Sh bilioni 20.

  Kitendo hicho cha staili ya Lowassa hakikutokea kwa Aveva pekee, pia ilitokea kwa Mwakilishi wa TFF, Wallace Karia aliyepita mbele na akatoa salamu kwa kutamka Simbaaa na wanachama wakaitikia mabadilikooo.
  Hali hiyo, ilikuwa ikitokea kila wakati pale wanachama au viongozi wakipita mbele ya ukumbi kwa ajili ya kutoa salamu ya kutamka Simba badala ya kuitikia oyeee, wanachama wakawa wanatamka mabadilikooo.
  Aina hiyo ya ushangiliaji iliendelea hadi mwisho wa mkutano huo saa 7:00 mchana mara baada ya Aveva kufunga mkutano huo.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku