• Breaking News

  Aug 1, 2016

  Kijana Mtanzania anayeichezea Timu ya Taifa ya Ureno(U-17)

  Anaipenda Tanzania kwa kuwa amezaliwa Tanzania na wazazi watanzania wanaoishi Tanzania mpaka sasa lakini kwa kuwa Ureno wamemuamini sana na kumpa nafasi ya kuichezea timu yao ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 basi hilo ndilo Taifa analotaka kulichezea mpaka kwenye timu ya Taifa

  Wazazi wake ambao ni raia wa Tanzania kutokea sehemu za Pemba walimpa jina la Fahim Rashid lakini wareno wamembabatiza jina la Fahem Nascimento de Sousa Rasheed Fim.

  Katika mahojiana na mtandao wa Soka360, Fim anasema alizaliwa mwaka 2000 visiwani Pemba kabla ya kuanza safari ndefu ya kusaka mafanikio ya soka na kuishi ndoto zake za kuchezea klabu kubwa ya Uingereza ambayo ilipata umaarufu zaidi nchini Tanzania kutokana na ujio wa bilionea Abramovich na kocha wa mataji, Jose Mourinho.

  ” Nimezaliwa Pemba na siwezi kusahau asili yangu ndio maana hata haya mazungumzo tunayafanya kwa kiswahili licha ya kuwa nimeishi nje ya Tanzania kwa muda mrefu.”

  Makuzi sahihi ya Soka

  Licha ya umri wake mdogo, safari yake ya soka ni ndefu akipita katika nchi za Ufaransa alikopelekwa na shemeji yake, kisha akapelekwa kwenye akademi ya soka nchini Poland.

  Mtunzi mashuhuri wa vitabu vya fasihi ya Kiafrika, hayati Chinua Achebe aliandika katika kitabu chake cha ” Things Fall Apart” kuwa ‘ A chick that will grow into a cock can be spotted the very day it hatches’. Kauli hii inadhihirika katika maisha ya soka ya Fim ambaye kipaji chake kilionekana na mgunduzi vipaji raia wa Ufaransa kipindi kifupi tu tangu atue Ufaransa licha ya umri wake mdogo.

  Mgunduzi huyo wa vipaji alitaka kumpeleka kwenye akademi ya klabu ya Bordeaux lakini hakufanikiwa ndipo alipoamua kumpeleka Poland.

  Mwaka 2009 alijiunga na akademi ya klabu ya Sporting Lisbon iliyowaibua nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo na Luis Nani.

  Akiwa katika akademi ya Sporting Lisbon, Wareno walichizika na uwezo wake kiasi cha kumpa jina jipya la kireno na kumpa nafasi ya kuchezea timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17.

  ” Nimeichezea timu ya taifa ya Ureno ya chini ya miaka 17 mechi moja ya kimataifa dhidi ya Poland. Kama si majeraha niliyopata wakati wa mazoezi niliyofanya Kigamboni Beach wakati nikiwa likizo jijini Dar mwezi uliopita basi ningekuwa nimefikisha mechi nyingi zaidi. ”

  Akiwa tayari ameshaichezea timu ya taifa ya Ureno ya chini ya miaka 17 na anasema ndoto yake ni kuichezea timu ya taifa ya wakubwa.

  ” Mipango yangu ni kuchezea Ureno kwa sababu wameniamini na nina nafasi kubwa ya kucheza”

  Utitiri wa vipaji vya Ureno havimtishi yeye kuamini kuwa lengo lake la kuvaa jezi za timu ya taifa ya wakubwa litatimia.

  ” Nitapata tu nafasi. Kuna wakati tunafanya mazoezi na nyota waliopita hapa, kina Figo, Ronaldo na Nani na hawa waliopo sasa, naona nitapata nafasi. ”

  Nafasi uwanjani

  Anaweza kucheza katika wingi ya kushoto na kulia huku akichezeshwa kama kiungo nambari 10 katika baadhi ya mechi kutokana uwezo wa kutumia miguu yote.

  ” kiasilia natumia mguu wa kulia lakini natumia miguu yote tena kwa nguvu sawa kabisa ndio maana naweza kucheza pande zote.”

  Anaitamani Chelsea

  Kinda huyo anaelezea kuwa sio tu ana ndoto za kuichezea timu ya taifa ya Ureno ya wakubwa bali pia anaweka wazi hisia zake za kuwa na malengo ya kuchezea klabu ya Chelsea.

  Japo haweki wazi sana lakini shauku ya kuichezea Chelsea inaweza kuwa inatokana na kuwa chini ya wakala mmoja na nyota mpya aliyetua Stamford Bridge hivi karibuni, Michy Batshuayi.

  Akademi ya Barcelona, La Masia ilitaka kumchukua lakini hakupendelea ofa yao kwa kuwa ana kiu ya kutaka kuanza kucheza mechi za ushindani katika daraja la kwanza kuliko kukaa akademi.

  Na kwa kuwa umri wake mdogo haumruhusu kucheza ligi kuu ya Ureno, Sporting Lisbon wamemtoa kwa mkopo wa msimu mzima kwenda katika klabu ya G Esporte Clube ambako anaamini atapata fursa ya kucheza na kukomaa zaidi

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku