• Breaking News

  Aug 9, 2016

  Kuhamia Dodoma Ghafla Kutafanyika Bila Madhara?

  WIKI chache zilizopita, Rais Dk John Magufuli alifufua ‘ndoto’ za mwaka 1973 za kuhamia Dodoma, zilizoanzishwa na aliyekuwa kiongozi wa nchi hii, Julius Nyerere.  Kama ilivyo kawaida, baada ya kulianzisha jambo hilo, wahusika wengi wakasema mara moja kwamba wako tayari kuhamia huko ambako ni karibu ya kila kona ya nchi.

  Tangu Nyerere aamue hivyo na uongozi wake, hivi sasa ni miaka 43 na hakuna lolote la kuonekana lililofanywa katika juhudi za kuhamia Dodoma, ukiacha shughuli za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge.

  Utawala wenyewe wa Mwalimu Nyerere ulikaa madarakani miaka ipatayo 12 baada ya tangazo bila kulitekeleza kikamilifu. Hata hivyo, ugumu wa utekelezaji wa suala hilo waweza kuwa ulichangiwa na uwepo wa vita vya Kagera.

  Serikali zilizofuata, za Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete pia zilishindwa kukamilisha jambo hilo zaidi ya kulizungumzia mara chache lakini bila utekelezaji.

  Kilichokuwepo ni wahusika kwenda Dodoma kwenye mikutano ya CCM tu na bungeni, baada ya hapo wanarejea Dar es Salaam kuendelea na maisha. Kwa watu waliozaliwa baada ya uamuzi huo na waliokuwa wadogo wakati ukitangazwa, mara zote wamekuwa wakibabaika kila wanapoambiwa Dodoma ndiyo mji mkuu wa Tanzania!

  Hivi leo baada ya Rais Magufuli kulifufua suala hilo, siyo tu mamilioni ya vijana wa nchi hii wanafahamu na kukumbuka kwamba makao makuu ya serikali ni Dodoma, bali na watendaji wa serikali, wazee kwa vijana, nao ndipo wanakumbuka kwamba walikuwa na wajibu wa kuhamia Dodoma.

  Pamoja na uamuzi huo wenye dhamira njema wa Rais Magufuli ambao umefanywa ‘kwa kushitukiza’, je, jambo hilo litafanyika kwa usalama, hususan kiuchumi?  Uamuzi huo wa kuwahamisha watu laki kadhaa kwenda Dodoma unaweza kweli kufanyika bila madhara kwa jamii ya Watanzania?

  Mbali na gharama za kibajeti, je, dhamira kwa wafanyakazi wa serikali kuhamia sehemu hiyo ya nchi ipo ama aliondoka nayo Nyerere?  Hii ni kutokana na ukweli kwamba hata wale waliokuwa wakifanya kazi na Mwalimu wakati huo na wakaendelea kufanya kazi na serikali zilizofuata, walionekana wazi kulipuuza suala hilo na kuendelea kuwekeza mali na makazi yao jijini Dar es Salaam.

  Miaka 43 iliyopita ni mingi ya kutosha ambapo tayari serikali ingekuwa imehamia Dodoma, licha ya nchi kutokuwa na rasilimali kubwa kama zilivyofanya nchi nyingine zilizohamisha makao makuu ya nchi zao.  Kilichokosekana katika miaka yote hiyo ni dhamira tu!  Nyerere alipoondoka madarakani, aliondoka na ‘Dodoma’ yake.

  Pamoja na uamuzi huo mwema ambao umefanywa mwaka huu wa 2016 ni matarajio ya raia kwamba hautaleta madhara au mzigo mwingine kwa mwananchi wa kawaida ambaye hivi sasa tayari anabeba ‘msalaba’ mzito wa kujinusuru na ukali wa maisha.

  Utayari wa kwenda Dodoma ambao kila mhusika amegundua kwamba anao – baada ya kupita miaka 43 – ufanyike salama na kumwacha Mtanzania maskini akiwa salama, kisiasa, kijamii na kiuchumi!

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku