• Breaking News

  Aug 20, 2016

  Lusinde Ang’ata na Kupuliza kwa Magufuli

  Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Balozi Job Lusinde amemtaka Rais John Magufuli kuzidisha ukali katika utendaji wake, lakini akakosoa mchakato wa kuuza nyumba za Serikali uliofanywa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

  Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake Uzunguni mjini hapa, Lusinde aliyeteuliwa kuwa waziri mara baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961, aligusia uamuzi wa kuuza nyumba za Serikali, akisema haukuwa sahihi.

  Hata hivyo, Lusinde, ambaye alikuwa waziri kwa miaka 15 wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema hilo suala si la kujadili tena kwa kuwa lilishapita.

  Nyumba za Serikali ziliuzwa wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, aliyeongoza nchi kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, wakati huo Rais Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi.

  “Ni kweli, mimi naona haikuwa sawa, zile nyumba za Serikali ziuzwe kwa namna ile. Kama walitaka kuuza basi wangeuza kwa nia ambayo ingewapa nafasi hata watu wengine (kununua),” alisema Lusinde.

  “Nafikiri wangetafuta tu hela ya kukarabati nyumba zote, kuliko sasa hivi tumeingia kwenye matatizo makubwa.”

  Hata hivyo, Lusinde hakutaka kujikita kwenye suala hilo ambalo lilisababisha mjadala mkubwa baina ya wanasiasa waliokuwa wakidai kuwa uuzwaji ulikuwa na harufu ya ufisadi. “Lakini sasa ‘that is not my issue now’ (hilo siyo suala langu tena). Sasa tuko kwenye hali hiyo ‘how do we do (tunafanyaje)?” alihoji Balozi Lusinde.

  “Mimi nafikiri tuangalie utekelezaji wa sera. Is it an issue (je, ni jambo muhimu) kwamba tuliuza nyumba za Serikali? Is it an issue (la hasha)? To me it’s not an issue. Tuangalie tunakokwenda. Whether it was correct or not, it is not an issue (kwamba lilikuwa ni jambo kubwa au la si hoja).”

  Lakini Lusinde, ambaye aliwahi kushika Wizara ya Mambo ya Ndani na pia kuwa balozi nchini China, alitofautiana na wanasiasa wanaonusa harufu ya rushwa kwenye suala la uuzwaji nyumba, akisema hakukuwa na ufisadi.

  “Nyumba za Serikali zilianza kuchakaa, sasa wakafikiria, wengine walikuwa humo, lakini nadhani haikuwa sawa. Wangezikarabati. (Badala yake) Wakasema ziuzwe kwa watumishi wa umma,” alisema.

  “Ni sawa na kusema magari mabovu, wauzieni watumishi wa Serikali. Kuna kitu kama hicho? Eti ni incentive (motisha), ya nini? Hakuna kitu kama hicho. Unamuuzia mtumishi wa Serikali, halafu yeye anaiuza kwa hela nyingi sana.”

  Alisema hata kama suala lilikuwa ni kuwauzia watumishi wa umma, ilitakiwa kuangalia wangapi watafaidika.

  “Lakini hii incentive sikubaliani nayo. Hata huko kwenye mashirika ninayoyaongoza hatukukubali kuuza mali ya mashirika, hakuna incentive yoyote,” alisema.

  “Mimi nilisema uza kwenye ‘open market’ (soko huria), pata pesa, tupate vitu vya kusaidia watu wote. Hata hivyo ilikuwa sera. It is not our issue (Si suala letu). Our issue ni sasa kuna ufisadi na ukwepaji wa kodi na kwa sababu Magufuli alikuwa serikalini, anajua wapi kuna tatizo.”

  Japo Lusinde alisema si sawa kulinganisha tawala zilizopita na utawala wa sasa, alisema kila utawala ulikuwa na mambo yake mema.

  “Hata Rais Ali Hassan Mwinyi alisema kila zama na kitabu chake. Unatazama majukumu gani, kulikuwa na nini wakati wa kupata uhuru? Nini kilitakiwa kifanyike? Serikali ilikuwa imetumwa kufanya nini wakati ule? Kuna mambo yanatakiwa kufanywa au kusahihishwa?” alisema.

  Alisema Mwalimu Nyerere alisisitiza zaidi kusaidia maendeleo ya vijijini, jambo linalofanyika hadi leo.

  “Katika utawala wa Jakaya Kikwete amejenga sana uhusiano na nchi za nje. Katika hali hiyo hiyo, huyu aliyeingia naye anafanya upande mwingine,” alisema.

  Hata hivyo, alisema wakati wa utawala wa Mkapa mambo ya utandawazi yalisababisha kuwe na vitendo vya ufisadi.

  “Katika miaka iliyofuata, mambo ya ufisadi yamekuwa mambo ya rushwa, mambo ya kutojali mali ya umma. Mambo hayo yalikuwa yanakua taratibu mpaka sasa yamekuwa makubwa. Sasa ni lazima tupambane nayo,” alisema.

  Amsifu Rais Magufuli

  Akizungumzia utawala wa sasa, Lusinde, ambaye aliwahi kuukosoa waziwazi utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne kuwa ulididimiza uchumi na kulea mafisadi, alimsifu Rais Magufuli na kumtaka aendelee na ukali aliouonyesha tangu aingie madarakani mwaka jana. “Mimi binafsi naunga mkono ukali wa Magufuli kwa mambo ya hovyo yanayofanyika. Kwa kweli tunahitaji ukali ili turudishe nidhamu ya Serikali na kuwa kinyume na uovu,” alisema Lusinde.

  Hata hivyo, alishauri kufanyika kwa marekebisho ya sheria zinazoonekana kukwazwa na ukali huo wa Rais katika kupambana na ufisadi.

  “Wakati wa kupambana nao, lazima kuwe na mikakati ya kufanya. Kuna vitu vingine kwa kutumia sheria zilizopo, itakuwa si rahisi kupambana navyo,” alisema Lusinde ambaye alimkabidhi mshale Rais Magufuli siku ya kuapishwa Novemba 5 mwaka jana.

  “Kwa hiyo itabidi Serikali itazame sheria zipi zinazuia mapambano yasiende kwa kasi ili ziangaliwe upya na mapambano yaende kwa kasi. Zile sheria tuzibadilishe,” alisema.

  “Mimi ningependa awe even a big ‘dictator’ (dikteta mkubwa zaidi) kwa miaka miwili, mitatu ili kuweka mambo sawa, kisha tuendelee kwenye sahani safi. Maana kuna mambo mengine inabidi utumie nguvu kubwa, mengine unatumia maji na mengine acid.”

  Kuhusu malalamiko ya vyama vya upinzani ya kuminywa kwa demokrasia, Lusinde alisema kwa sasa siasa hazitakiwi.

  “Ni sawa, katiba inakubali, lakini lazima tuangalie, hivi tutakuwa watu wa siasa tu? Sisi tumefundishwa na Mwalimu (Nyerere) tukienda vijijni tunakuta siasa, kila kitu kinageuzwa kuwa siasa. Yaani sasa inakera. Jambo lilikuwa jema, lakini linageuzwa kuwa la kisiasa,” alisema.

  “Ujengaji wa uchumi hautaki siasa. Sasa tukazane na maendeleo. Viongozi fanyeni kwa vitendo. Hizi siasa za mikutano na maandamano (tuziache). Hebu sasa twende pamoja.”

  Bunge

  Kuhusu utendaji wa Bunge, Lusinde alimsifu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akisema amejitahidi kusimamia kanuni za Bunge na kuwadhibiti wapinzani waliozikiuka.

  “Hata mimi nimeshakuwa mbunge kwa miaka 15 na waziri, na kujibu maswali kwa miaka 15. Kuna vitu ambavyo Bunge lina uhuru mkubwa wa kujitengenezea mambo, vile vile kuna nidhamu yake,” alisema.
  “Kanuni zipo, ziheshimike. Anayetakiwa kuhakikisha kuwa zinaheshimika ni Spika. Nilikuwa naangalia trend (mwelekeo wa) za bajeti za miaka miwili hadi mitatu iliyopita. Spika anasimama na wewe unaendelea kusimama, anakwambia uketi chini, hutaki? Huo ni uhuni,” alisema.
  “Sasa Tulia anasema kama tumefikia huko, tuendelee kufuata kanuni. Anasema atakutaja, akikutaja inabidi uende kwenye Kamati ya Nidhamu. Mimi nafikiri Tulia amejitahidi kuleta nidhamu katika Bunge,” alisema.

  Kuhusu mwafaka unaotarajiwa kufanywa na Spika Job Ndugai kati ya vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema ni sawa lakini wao ndio wenye makosa.

  “Walichofanya Ukawa si sawa kwa sababu wao ndio walivunja sheria. Lakini hali imekwenda hivyo, mnafanyaje? Mnatafuta mwafaka. Sasa tujiulize ni mwafaka wa aina gani? Kwa sababu huwezi kumhukumu Tulia kwa kazi yake nzuri,” alisema.

  “Ni kweli hawa ndiyo wamefanya kitu ambacho si kizuri, lakini you open a door somewhere (unafungua mlango sehemu fulani), nao waingie,” alisema.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku