• Breaking News

  Aug 6, 2016

  Mkuu wa Mkoa wa DSM Paul Makonda Apiga Marufuku Maandamano ya UKUTA, Awapa Rungu FFU

  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwepo kitu kinaitwa UKUTA ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.

  Akizungumza na kikosi cha kutuliza ghasia katika kambi ya Ukonga Jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa amesema kwa kuwa askari wanafahamu sheria wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo au maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaagiza kinachotakiwa ni utekelezaji.

  ‘’Msisubiri maelekezo yoyote kutoka juu, asiwepo mtu yeyote atafunga duka kwa sababu ya UKUTA nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza kusimama mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini hatutakuwa na vurugu kwenye Mkoa wetu na hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua madhara ya vurugu’’ Amesema Makonda.

  Aidha kwa upande wake Kamanda wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas Mkondya amesema jeshi la polisi lipo vizuri na vijana wameandaliwa vizuri na wameandaliwa kuwa tayari siku nyingi na hakuna mtu yeyote atakayethubutu kufanya UKUTA na watakaofanya hivyo watazimwa kabla hawajafanya chochote.

  Kamada amewataka wananchi wote Jijini Dar es Salaam kuto jitokeza kwenye oparesheni UKUTA kwa kuwa maandamano hayo siyo halali na watakaojitokeza watapata matatizo yasiyowahusu.

  Oparesheni UKUTA ilitangazwa na CHADEMA ikiwa na maana Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania na ikatajwa tarehe Mosi Septemba nchi nzima chama hicho kitafanya mikutano ya hadhara jambo ambalo limepingwa na serikali kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufuatia wakuu wa mikoa.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku