• Breaking News

  Aug 11, 2016

  Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Akifuta Chama Kimoja Leo...

  Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi amekifuta katika orodha ya vyama vya siasa vyenye usajili wa muda Chama cha Maadili na Uwajibikaji (CM-Tanzania), kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya usajili.

  CM Tanzania kilipata usajili wa muda tarehe 4 Februari na kutakiwa kuendelea na taratibu za kutimiza masharti kwa ajili ya kupata usajili wa kudumu.

  Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msajili na kusainiwa na Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza imeeleza kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992, chama cha siasa chenye usajili wa muda ni lazima kiwasilishe maombi ya usajili wa kudumu ndani ya siku 180 tangu tarehe ya kupatiwa usajili wa muda.

  Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa chama cha siasa chenye usajili wa muda, usajili wake unaisha baada ya siku 180 tangu kipate usajili wa muda.

  “Hivyo uhai wa cheti cha usajili wa muda wa Chama cha Maadili na Uwajibikaji (CM-Tanzania) ulikwisha tarehe 02 Agosti, 2016, kwani waanzilishi wake walipaswa kuwasilisha maombi ya usajili wa kudumu siyo zaidi ya 02 Agosti, 2016” Imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

  Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa kwa mujibu wa sheria, waanzilishi na wanachama wote wa chama hicho hawapaswi kufanya siasa au shughuli yoyote kwa jina la chama hicho na kufanya hivyo ni kukiuka sheria.

  Kufutwa kwa CM-Tanzania kunafanya idadi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa muda kuwa kimoja ambacho ni Chama cha Restoration of the Nation Party (RNP).
  Aidha vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vimeendelea kuwa 22.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku