• Breaking News

  Aug 6, 2016

  Mwenyekiti Atuhumiwa Kumpa Mimba Mwanafunzi

  POLISI mkoani Mwanza inamshikilia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sangabuye, Kata ya Igombe katika Manispaa ya Ilemela, John Mayala (38) akituhumiwa kumtorosha na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili (jina linahifadhiwa) wa Shule ya Sekondari ya Sangabuye.

  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa mtuhumiwa anatuhumiwa kutenda kosa hilo Agosti 3, mwaka huu katika mtaa huo.

  Aliongeza kuwa Polisi inamshikilia pia mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Agnes Kadilana (47) ambaye pia ni mkazi wa mtaa huo kwa kushindwa kuwapatia ushirikiano polisi mara baada ya kuhojiwa na kukana kuwepo kwa tukio hilo.

  Aliwataka wanaume wenye uroho wa kufanya mapenzi na watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka 18, kuacha mara moja kwa madai kuwa, kwa kufanya hivyo watakuwa wametenda kosa la ubakaji.

  Aidha, katika tukio lingine, Kamanda Msangi alisema Polisi imekamata silaha aina ya Rifle muundo wa Mark 4 yenye namba za usajili 3989529 nyumbani kwa Msafiri Suleiman ambaye alikuwa mtuhumiwa wa ujambazi wa unyang’anyi wa silaha aliyeuawa kwa kupigwa risasi miguuni na askari wakati akijaribu kutoroka.

  Katika tukio lingine, Kamanda Msangi alisema Polisi imemkamata mtuhumiwa wa mauaji na uporaji wa pikipiki katika Jiji la Mwanza, Moses Elias Makaro (42), mkazi wa Mtaa wa Kamaliza wilaya ya Nyamagana.

  Alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa na pikipiki yenye namba za usajili MC 608 ADD aina ya SAN LG ambayo ilitambuliwa kuwa ndiyo aliyoporwa Shaban Haruna aliyeuawa Julai 20, mwaka huu maeneo ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku