• Breaking News

  Aug 18, 2016

  Rais Magufuli, Unateua Kwa Lengo la Kupambana na Wapinzani au Kuleta Maendeleo?

  Rais Magufuli
  Mhe. Rais,una sera nzuri za kimaendeleo. Ilani yetu ya CCM,ahadi zako za papo kwa papo,kauli zako na matendo yako huakisi maendeleo ya Tanzania yetu. Kuwa Tanzania ya Viwanda. Lakini,teuzi zako hazibebi lengo lako hilo. Zinabeba dhima tofauti ya kupambana na kuwabana wapinzani hasa CHADEMA.

  Natoa mifano mitatu. Wa kwanza ni uhusuo uteuzi/kupandishwa cheo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda. Makonda alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Tangu akiwa UVCCM,Makonda hujichora kama mpambanaji wa wapinzani na kwake hawafurukuti. Kinondoni UKAWA 'wakamtandika' kwa kutwaa majimbo yote. Rais ukasema mahali kuwa Makonda ana wapinzani wengi wanamchukia. Ukaahidi kumpandisha cheo. Ikawa kweli. Ameshaapa kuubomoa UKUTA wa CHADEMA wa hapo Septemba mosi!

  Mfano wa pili ni uteuzi wa maDED na maDAS. Humo wamesheheni walewale wenye hulka na michoro ya kupambana na wapinzani. Watoa matamko ya kuponda bila kupenda wapinzani ndiyo wameula kwenye teuzi hizo. Matamko yao humu JF,WatsApp,Facebook na Instagram kuwakandiakandia wapinzani yakawalipa.

  Mfano wa tatu ni wa uteuzi wa leo wa Mrisho Gambo. Umetengua uteuzi wa kaka Ntibenda na kumpandisha cheo kwa kumteua Mrisho Gambo kuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha. Mrisho Gambo alijaribu kugombea Ubunge Kinondoni. Akabwagwa na Idd Azzan ndani ya CCM yetu. Ni juzi tu amejigamba kuwa yeye ndiye kiboko ya Operesheni UKUTA ya CHADEMA kule Arusha. Gambo amejipambanua kuwa yuko Arusha kupambana na wapinzani wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless J Lema.

  Nia ya teuzi hizi ni ipi hasa? Maendeleo au 'kuwafunika' wapinzani?

  Mzee Tupatupa wa Lumumba,Dar es Salaam

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku