• Breaking News

  Sep 22, 2016

  BODI Inayosimamia Gazeti la Uhuru, Mzalendo, Uhuru FM Yajiuzulu..Kisa Hichi Hapa

  Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambavyo ni Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa Gazeti la Uhuru, Mzalendo na Burudani pamoja na Peoples’ Media Communication Limited (PMCL) inayoendesha kituo cha redio Uhuru imejiuzulu kupitia barua ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo Al-haj Adam O. Kimbisa.

  Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli amepokea barua ya kujiuzulu kwa bodi hiyo leo tarehe 22 Septemba 2016 ambayo nakala yake imenakiliwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana.

  Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, barua hiyo inaeleza kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa Bodi hiyo wameamua kwa hiyari yao kujiuzulu nafasi zao.

  Bodi ya Uhuru Media Group ndiyo iliyokuwa na majukumu ya kusimamia, kuzielekeza na kuzishauri Menejimenti ya Makampuni hayo na kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vyombo vya habari vya Chama.

  Kujiuzulu kwa bodi hiyo kumekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Uhuru Publications.

  Kwenye ziara hiyo, wafanyakazi walilalamika kutolipwa mishahara yao kwa miezi saba, kutotolewa kwa michango ya wafanyakazi kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii, Kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti katika hali ya kutatanisha, kutotambuliwa katika ajira kwa baadhi ya wafanyakazi, kutolipwa kwa madeni wanayozidai taasisi za serikali na wanaostaafu kutolipwa mafao yao.

  Wafanyakazi hao pia walimueleza Rais Magufuli kuwa Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya vyombo vya habari vya chama inayoendesha Gazeti la Uhuru na Uhuru FM zimeshindwa kuendesha vyombo hivyo na wamemuomba aingilie kati ili kuvinusuru vyombo hivyo ambavyo kwa sasa vina hali mbaya kutokana na kukabiliwa na madeni makubwa, na biashara yake kushuka kwa kiasi kikubwa.

  Rais Magufuli alimuagiza Katibu Mkuu wa CCM, ABDULRAHAMAN KINANA kuhakikisha mishahara yote wanayodai wafanyakazi inayofikia shilingi milioni- 609 inalipwa ndani ya mwezi huu na pia kuagiza kupatiwa orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa na Magazeti ya Uhuru na Mzalendo.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku