• Breaking News

  Sep 4, 2016

  HAYA Hapa Maoni Mbali Mbali ya Wataalamu wa Uchumi Baada ya Rais Magufuli Kutishia Kubadili Fedha

  Rais Maguful
  Dar es Salaam. Baadhi ya wachumi nchini wametofautiana kuhusu kauli ya Rais John Magufuli kutishia kubadili fedha ili kuwadhibiti watu wenye tabia ya kuzificha, huku Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu akisema kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi inajitosheleza na hawezi kutoa tafsiri yoyote.

  Wakati Profesa wa Uchumi, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi akisema haamini kama fedha zilizofichwa ni nyingi kiasi cha kuteteresha mzunguko wa fedha nchini na kutaka zitizamwe sababu za fedha kutoonekana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT) mkoani Iringa, Dk Bukaza Chachage alisema kuficha fedha kwa nia ovu ni kosa kubwa kwa sababu huhatarisha uchumi.

  Katika maelezo yake, Profesa Ngowi alisema ili kubadili fedha ni lazima kuweka matangazo ili wale wenye fedha zinazotaka kuondoshwa katika mzunguko waweze kuzitoa na kubainisha kuwa moja ya sababu ya kuzibadili ni kuongezeka kwa fedha bandia.

  Rais Dkt Magufuli atishia kubadili fedha.

  “Ili kuwadhibiti watu wanaoficha fedha, suluhisho si kuchapisha au kubadili fedha. Binafsi siamini kama kuna watu wameshika mabilioni kiasi hicho,” alisema na kuongeza: “Hapa suala la kutazama ni sababu za fedha kufichwa au kutoonekana. Unajua Serikali hii imebana matumizi, ukusanyaji kodi kwa sasa umeimarika, safari zimepungua kwa kiasi kikubwa, sekta binafsi nazo zinakosa fedha kwa kuwa Serikali imeanzisha utaratibu mpya, kama vikao kutofanyia katika mahoteli.”

  Katika hilo, Dk Chachage alisema: “Ukificha fedha ndani maana yake bidhaa zinakuwa na bei kubwa na mahitaji ya fedha pia yanaongezeka kwa kasi na suala la kupata fedha linakuwa ngumu. Benki zinakosa fedha, hata kukopa pia hushindikana. Hapo suluhisho ni kuwabana wahusika kuziachia ili kuwe na mzunguko wa fedha unaokidhi utashi wa watu wote. Hilo la kubadili huwa hatua ya mwisho.”

  Alisema uwepo wa fedha bandia ni sababu kubwa kwa Serikali kubadili fedha na kusisitiza kuwa watu wengine huamua kuficha kwa sababu zinakuwa za wizi.

  Hata hivyo, mwanazuoni wa uchumi, Profesa Samwel Wangwe aliishauri BoT kuzungumzia jambo hilo kwa sababu kufanyika kwake ni lazima ijadiliane na Wizara ya Fedha.

  Chanzo: Mwananchi.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku