• Breaking News

  Sep 27, 2016

  HOJA: Msajili wa Vyama vya Siasa ana Mamlaka kufanya alichofanya kwa Lipumba na CUF?

  Kuna baadhi ya watu(wakiwemo viongozi wa CUF) wanadai kuwa, Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya chama cha siasa, hivyo msimamo wake juu ya mgogoro wa uongozi wa chama cha CUF ni batili.

  Msajili wa hana mamlaka ya kuingilia uamuzi halali uliofanywa na kikao halali cha chama cha siasa, Lakini, kama uamuzi ni batili na kikao ni batili au uamuzi ni halali umefanywa na kikao batili au uamuzi batili umefanywa na kikao halali, msajili hawezi kuutambua, kwani Sheria ya Vyama vya Siasa inampa Msajili wa Vyama vya Siasa wajibu wa kusimamia utekelezaji wa baadhi ya maamuzi ya chama cha siasa ikiwamo suala la upatikanaji wa viongozi wa kitaifa wa chama cha siasa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama husika.

  Ni vyeme ieleweke kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa uamuzi wa kufanya mabadiliko yoyote kwa viongozi wa kitaifa wa chama cha siasa ni lazima upelekwe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ili atambue mabadiliko hayo.


  uala la uanachama wa chama cha siasa ni uhusiano wa kimkataba uliopo kati ya mwanachama na chama chake. Hivyo, endapo mwanachama anayechukuliwa hatua za kiidhamu siyo kiongozi wa kitaifa wa chama cha siasa, basi Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia mgogoro huo wa uanachama., labda chama cha siasa na mwanachama husika kwa hiari yao wamuombe Msajili wa Vyama vya Siasa kuwasuluhisha.

  Isipokuwa, endapo mwanachama husika ni kiongozi wa kitaifa wa chama, basi Msajili wa Vyama vya Siasa anayo mamlaka ya kuingilia mgogoro huo ili kujiridhisha kuwa, mwanachama husika amesimamishwa au kufukuzwa uanachama wake kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za chama husika, kwa sababu kusimamishwa au kufukuzwa uanachama wake kunaathiri nafasi yake ya uongozi wa kitaifa.

  HITIMISHO

  Kwa kuwa kifungu cha 10(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 kinahitaji chama cha siasa kuwasilisha orodha ya viongozi wake wa kitaifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

  Na kwa kuwa kifungu 8A(1) kinampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuhifadhi taarifa za viongozi wa kitaifa wa Vyama vya Siasa na kwa kuwa pia Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa toleo namba 111 la mwaka 1992, inakitaka kila chama cha siasa kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa panapotokea mabadiliko katika uongozi wa taifa.

  Aidha, Msajili wa Vyama vya Siasa kwa mantiki ya majukumu yanayobebwa na vifungu hivyo, anao wajibu wa kuhakikisha taarifa za mabadiliko ya uongozi anazoletewa na chama cha siasa ni sahihi, kwa maana ya kujiridhisha kuwa mabadiliko hayo ya uongozi, yamefanywa na mamlaka halali ya chama na pia yametekelezwa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama husika. Hatua hiyo inafanyika, ili kuepuka kupokea na kuhifadhi taarifa ya mabadiliko katika uongozi wa kitaifa wa chama cha siasa ambayo siyo halali, kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama husika.

  Kwa mantiki hiyo basi, tukijielekeza kwenye vifungu vya Sheria vilivyoainishwa hapo juu, ni dhahiri kwamba, Msajili wa Vyama vya Siasa anayo mamlaka na wajibu wa kisheria, kuchunguza mabadiliko katika uongozi wa kitaifa wa chama yaliyofanyika na masuala yote yanayohusu na mabadiliko hayo. Mfano, pale ambapo mwanachama ni kiongozi wa kitaifa wa chama cha siasa Msajili anapaswa kujiridhisha kuwa, mwanachama husika amesimamishwa au kufukuzwa uanachama kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za chama, kwa sababu kusimamishwa au kufukuzwa uanachama wake, kunaathiri nafasi yake ya uongozi wa kitaifa.

  Nimeipata toka sehemu

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku