• Breaking News

  Sep 7, 2016

  Jukumu la Kulea Watoto ni la Wazazi..Serikali Haina Mpango wa Kuanzisha Vituo vya Watoto-Waziri

  Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla nchini Tanzania, wametakiwa kubeba jukumu la malezi kwa watoto ili kuwapa haki zao stahiki ikiwa ni pamoja na kupunguza tatizo la watoto wa mitaani na wanaoishi katika mazingira magumu.

  Akizungumza leo Bungeni Mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla amesema kuwa serikali kwa sasa haina mpango wa kuanzisha vituo vya watoto hao kwani jukumu la watoto kwa serikali ni hatua ya mwisho kabisa.

  Dkt. Kigwangala amesema kuwa endapo mtoto atafiwa na wazazi wake basi familia inapaswa kushikilia malezi ya mtoto na kama familia haina uwezo basi jamii inayomzunguka ina wajibu wa kufanya hivyo ili kuwapa watoto wa aina hiyo malezi bora zaidi.

  Amesema kuwa wizara hiyo pia inaendelea na kutekeleza mpango wa ulinzi wa mtoto wa mwaka 2013/2017 katika jitihada za kuboresha malezi ya watoto kwa kuimairisha mfumo wa malezi na matunzo ya watoto katika ngazi ya familia na jamii.

  Akisisitiza zaidi kuhusiana na msimamo wa serikali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wabunge kwa pamoja kushirikiana na mabaraza yao ya madiwani kuweka mikakati ya kupunguza watoto wa mitaani kwa kushauri ni jinsi gani ya kuweza kuwawekea ulinzi na maisha yao ya baadaye.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku