• Breaking News

  Sep 11, 2016

  Kasi ya ongezeko la wanawake kuzaa kwa upasuaji

  Huenda ujana, urembo na usasa ukachagiza kasi ya ongezeko la kina mama wanaojifungua kwa upasuaji.

  Chagizo hilo linatokana na kuwapo kwa ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa upasuaji, lakini matakwa ya baadhi ya wanawake kuomba kufanyiwa upasuaji hata bila kuwa na sababu yatachangia ongezeko hilo.

  Baadhi ya wanawake waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema kuwa hawataki shida ya kuteseka na uchungu wakati wa kujifungua, kutanuka maumbile yao, hivyo hulazimisha wafanyiwe upasuaji.

  Mbali na sababu hizo zipo za kuchoka kubeba mimba na kukwepa kero za wauguzi.

  Jacqueline Swai (jina la baba siyo halisi) anasema kuwa alipanga na mumewe kuzaa watoto watatu, hivyo alifahamu hatapata taabu akifanyiwa upasuaji kwa sababu hatahitaji kufanyiwa mara nyingi.

  Anasema walikuwa anasikia mwanamke kujifungua kwa upasuaji mwisho mara tatu na kwa sababu mumewe alimueleza anahitaji watoto watatu akaona haina haja ya kuteseka na uchungu.

  Anafafanua alikuwa na daktari maalumu kwa ajili ya kufuatilia ujauzito wake hivyo walikubaliana mapema kuwa utakapofika wakati wa kujifungua afanyiwe upasuaji.

  “Mume wangu tulimdanganya kuwa nina matatizo hivyo ni bora nifanyiwe upasuaji, alikubali kwa sababu tulicheza mchezo huo na daktari,” anasema.

  Ilinda Moses anasema alipojifungua mtoto wa kwanza aliteseka siku mbili ikiwamo kutundikiwa maji ya uchungu, kuwekewa kidonge cha uchungu bila mafanikio na akafanyiwa upasuaji.

  Alisema baada ya mateso hayo yote ya kuvumilia maumivu siku mbili bado alifanyiwa upasuaji jambo ambalo halitaki tena na wala hatakaa na mimba miezi tisa kama awali badala yake akichoka anaomba kufanyiwa upasuaji.

  Kwa mujibu wa taasisi ya matibabu ya nchini Marekani iitwayo The National Center for Biotechnology Information (NCBI) inayofanya kazi kwa kushirikiana na maktaba ya dawa ya nchini humo iitwayo The United States National Library of Medicine (NLM), imezindua utafiti unaoelezea kuongezeka kwa upasuaji kwa kina mama wanaojifungua.

  Utafiti huo uliochapishwa pia katika jarida la Medicine Journal uliofanywa katika nchi 150 ikiwamo za Afrika na uliofanywa kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2014 umelibaini hilo.

  Utafiti huo umeonyesha kuwa

  Kwa mujibu wa takwimu zilizomo kwenye utafiti huo zinaonyesha kuwa kwa sasa asilimia 18.6 ya watoto wote huzaliwa kwa upasuaji, huku asilimia 6 hadi 27.2 hutokea katika mikoa iliyoendelea.

  Utafiti huo ulionyesha Amerika Kusini na Caribbean watoto waliozaliwa kwa upasuaji ni asilimia 40.5, ikifuatiwa na Amerika ya Kaskazini asilimia 32.3, Ulaya asilimia 25, Asia asilimia 19.2 na Afrika asilimia 7.3.

  Kulingana na takwimu zilizofanywa kwa nchi 121 zaidi zilionyesha kuwa kati ya mwaka 1990 na 2014, kiwango cha watoto wanaozaliwa kwa upasuaji kiliongezeka kwa asilimia 12.4 , kutoka asilimia 6.7 hadi 19.1 na kiwango cha wastani wa ongezeko la asilimia 4.4.

  Kiongozi wa utafiti huo Profesa Michael Smith anazitaja sababu walizobaini kupelekea ongezeko hilo kuwa ni wanawake wengi kutokubali kuvumilia kusukuma kwa njia ya kawaida.

  Anasema walipata sababu hizo kutokana na mahojiano waliyofanya na baadhi yao na pamoja na sababu hiyo nyingine ni kutotaka kuharibu maumbile kwa kile walichodai wakizaa kwa kawaida wataharibu mfumo mzima wa mwili wao.

  “Inashangaza wanawake wanapokuwa wajawazito wanatamani kupata mtoto tu bila kupitia taratibu husika jambo ambalo huwanyima haki watoto ikiwamo ya kunyonya maziwa ya mama,” anasema Profesa Smith.

  Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili za mwaka 2008/2009 zinaonyesha wajawazito 4,250 sawa na asilimia 44.7 walijifungua kwa njia ya upasuaji na mwaka 2009/2010 wajawazito 4,490 sawa na asilimia 48.

  Takwimu za Julai mwaka 2011 hadi Mei 2012 za Hospitali ya Amana kwa siku moja madaktari huwafanyia upasuaji wajawazito 10 hadi 11na kati ya Julai mwaka 2011 hadi Mei mwaka 2012, hospitali hiyo ya imefanya upasuaji kwa wajawazito 1,439.

  Takwimu za wajawazito

  Takwimu kutoka kwa vyanzo mbalimbali hapa nchini zinaonyesha kuwa kati ya wajawazito wanaojifungua kwa upasuaji, asilimia 82 hutaka wenyewe kwa sababu zao binafsi, huku waliobaki wakilazimika kufanya hivyo kutokana na matatizo ya kiafya.

  Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk Meshack Shimwela alisema kuongezeka kwa upasuaji kunatokana na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kupunguza vifo vya mama na mtoto.

  Dk Meshack ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, alisema WHO inazitaka nchi zinazoendelea kufikisha angalau asilimia 12 ya upasuaji.

  “Tunafanya upasuaji kwa kuwa, tunatakiwa tuokoe maisha ya mama na mtoto. Huduma za upasuaji zinatolewa bure ili kupunguza vifo hivyo,” alisema Shimwela.

  Alizitaja sababu zinazosababisha Hospitali ya Amana kufanya upasuaji kwa asilimia kubwa kuwa ni kutaka kufikia malengo ya WHO.

  “Tumepata chumba chenye vifaa vyote cha kufanyia upasuaji kwa hiyo tumeongeza huduma hiyo,” alisema.

  Aliongeza kuwa upasuaji huo hufanyika kama kuna sababu za msingi kama vile ukubwa wa mtoto na nyingine.

  Alisema sababu nyingine ambayo imesababisha kuwapo ongezeko la wajawazito kujifungua kwa upasuaji katika hospitali hiyo ya Amana ni hospitali ya rufaa, hivyo wajawazito wanaoshindikana katika hospitali ndogo huletwa hapo.

  Mtindo wa maisha

  Sababu nyingine kwa mujibu wa Dk Shimwela kutokana na mfumo wa maisha kama vile wajawazito kutofanya mazoezi kutozingatia masharti.

  “Wajawazito hawafanyi mazoezi, hawafuati masharti na elimu wanayopewa na wakunga. Siku hizi wanakula vizuri tofauti na zamani, kwa hiyo watoto wanakuwa wakubwa,” alisema.

  Sababu za wanawake kukwepa

  Gazeti hili lilizungumza na wanawake 12 ambao walitaja baadhi ya sababu zinazowafanya wachukie kuzaa kwa njia ya kawaida, ikiwamo kutotaka kuzeeka, kuogopa mateso ya uchungu, kuchoka kubeba mimba na kuogopa manyanyaso wakati wa kujifungua.

  Baadhi kutaka kubaki vijana

  Baadhi ya wanawake waliozungumza na gazeti hili walisema hawakutaka kuharibu maumbile yao kwa kuzaa kwa njia ya kawaida.

  “Ninachofahamu nikizaa kila kitu kitakuwa imekuwa cha uzazi uzazi, sitaki nataka nibaki kama nilivyo, licha ya matiti kuonyesha dalili za unyevunyevu wa kutaka kutoa maziwa hata mtoto wangu sikumnyonyesha,” anasema mmoja wa wachangiaji ambaye kwa kulinda heshima yake jina lake hakutaka liandikwe.

  Anasema siyo kwamba hafahamu maziwa ya mama ni bora kwa mtoto na akizaa maumbile yatarudi kama zamani anafahamu lakini kisaikolojia haoni hilo kama lipo sawa kwake kwa sababu bado ana safari ndefu ya kufurahia ujana.

  Kuogopa mateso ya uchungu

  Walio wengi kati ya hao walisema wamewahi kuzaa mara moja na kuona uchungu unavyotesa au wamewahi kuona wenye uchungu wa kujifungua wanavyoteseka na kutotaka wakutane na hali hiyo.

  Kuchoka kubeba mimba

  Wengine walisema wamechoka kubeba mimba hivyo kuamua kujifungua kabla ya muda, hivyo kulazimika kufanyiwa upasuaji.

  Manyanyaso wakati wa kujifungua

  Miongoni mwao wapo waliosema wamewahi hadi kupigwa vibao wakati wa kujifungua mimba zao za mwanzo hivyo kukwepa kero hiyo hawataki uchungu ambao husababisha wasumbuane na wauguzi wanachagua upasuaji.

  “Oooh...Nilitoka leba nikiwa na alama nyekundu mapajani, nililia sana wakati wa uchungu nikaishiwa nguvu, wakati wa kusukuma ulipofika nikawa siwezi nilichezea vibao siyo vya kawaida”.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku