• Breaking News

  Sep 25, 2016

  Madaktari wenye maduka nje ya hospitali kukiona


  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk Beatrice Byalugaba kufanya uchunguzi na kubaini madaktari wa Hospitali ya wilaya ya Mafia wanaomiliki maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo na kuwachukulia hatua.

  Amesema ameshangazwa kukuta maduka ya dawa yanayomilikiwa na madaktari nje ya hospitali hiyo kwani tayari Serikali ilishaagiza kuondolewa kwa maduka ya madaktari karibu na hospitali wanazofanyia kazi. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea Hospitali ya wilaya ya Mafia katika siku ya pili ya ziara yake wilayani humo.

  Kuhusu tatizo la upungufu wa dawa hospitalini hapo alimuagiza Dk Beatrice kufanya utafiti wa aina ya magonjwa yanayowasumbua wananchi wa wilaya hiyo ili wanapoagiza waagize dawa nyingi za kutibu magonjwa hayo.

  Pia aliwataka watumishi wa hospitali hiyo wajitahidi kuwahudumia vizuri wagonjwa licha ya uchache wao, lengo likiwa ni kuhakikisha wanapunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

  Wakati huo huo Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupatiwa matibabu bure kwa kipindi cha mwaka mzima.

  Awali Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk Joseph Mziba alisema mwamko wa wananchi kujiunga na Mfuko wa CHF ni mdogo jambo linalokwamisha upatikanaji wa huduma za afya wilayani Mafia. Jumla ya wananchi waliojiunga na CHF ni watu 6,000 kati ya watu 50,000.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku