• Breaking News

  Sep 11, 2016

  MTATIRO : Magufuli Atafanikiwa Kwa Kuambiwa Ukweli

  By Julius Mtatiro
  Katika taifa letu kumekuwa na mgawanyiko wa wazi juu ya utendaji wa Rais wa sasa, John Magufuli na Serikali yake.

  Lipo kundi linaamini kuwa kiongozi huyu ndiye mkombozi wa kipekee wa Tanzania na watetezi hao wana hoja za msingi. Moja ya hoja hizo ni kuwa, tangu kuondoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mtu ambaye amefuata nyayo zake ni JPM.

  Hata hivyo, upande huu unajenga hoja zaidi kwamba JPM ni kiongozi mwenye msimamo na anayetetea watu wanyonge, hana masihara na analisimamia Taifa kwa nia ya kuleta maendeleo yatakayomnufaisha kila mtu. Hiyo ni sifa moja, zinatajwa zingine nyingi.

  Lipo kundi la pili ambalo linaamini kuwa JPM ni kiongozi mzuri katika kuzungumza mipango mingi na kujenga ushawishi wa lazima kwa wananchi, lakini yeye na serikali yake wanakosa usimamizi shirikishi wa mipango hiyo.

  Kundi hili linamwona JPM kama kiongozi mkandamizaji na anayetamani mfumo wa demokrasia vya vyama vingi ufutwe hapa nchini. Kundi hili linao ushahidi kuanzia namna Bunge linavyodhibitiwa na Serikali ya JPM, vyombo vya habari na vyama vya siasa.

  Kundi hili linaamini kuwa JPM akishakamilisha mkakati wa kudhibiti maeneo hayo atahamia kwenye makundi mengine ya kijamii na mwisho wa siku raia wote nchi nzima watakuwa mfukoni mwa mtu mmoja. Mimi niko kwenye kundi hili la pili na kwa sababu hiyo nitaeleza kwa nini kundi la kwanza haliko sawasawa.

  Kumfananisha JPM na Mwalimu Nyerere

  Kwanza, kumfananisha JPM na Mwalimu Nyerere ni kufanya makosa makubwa. Mwalimu aliongoza nchi katika wakati wa uhuru, hakuwa na wasomi wengi, hakuwa na watendaji wenye weledi mkubwa.

  Mwalimu Nyerere kwa kiasi kikubwa alitaka kujenga Taifa lenye umoja, moja na linalojitambua na aliwekeza nguvu kubwa katika kuijenga Tanzania yenye kabila moja kati ya makabila zaidi ya 100. Pia, alitaka kuijenga Tanzania yenye dini moja kati ya dini na madhehebu yaliyopo.

  Kwenye hii ajenda ya dini Mwalimu alifanikiwa, dini kubwa ya Watanzania ni Utanzania wenyewe, ndiyo maana kokote kule uendako nchini, dini kuu halisi za nchi hii (Ukristo na Uislamu) zinafanya kazi pamoja katika masuala ya msingi.

  Ukifika misibani utakuta Wakristo na Waislamu wanazikana kama ndugu, kwenye sherehe za dini ya Kiislamu utaona Wakristo wakialikwa na zile za wakristo, waislamu wakialikwa.

  Ukienda katika maeneo kadhaa ya nchi, ni utamaduni wa kawaida kukuta hospitali ya kanisa ikitumiwa na wananchi wasio waumini wa dini hiyo.

  Kama ni hospitali ya kanisa Katoliki walokole wanatibiwa na Waislamu wanatibiwa. Unaweza kukuta hospitali ni ya shirika la Kiislamu au waamini wa kiislamu, lakini madaktari waliopo ni wakristo na wanaotibiwa hapo ni watu wa dini zote.

  Hii ndiyo Tanzania aliyokuwa anaijenga Mwalimu Nyerere. Utashi huo haukuishia kwenye mambo hayo, alijaribu kuujenga mpaka kwenye uchumi na mifumo yote ya maisha, kwamba kuwe na usawa kati ya maskini na tajiri katika kupata huduma za msingi za kijamii, lakini usawa huo uende hadi kwenye mifumo ya kisheria.

  Hata hivyo, kwa kiasi fulani na kwa baadhi ya maeneo, Mwalimu Nyerere hakufanya vizuri hasa kwenye uchumi, lakini jambo la msingi la kukubaliana ni kuwa, walau aliacha alama za masuala aliyoyasimamia.

  Wakati Mwalimu Nyerere akipambana na mazingira ya ujenzi wa mifumo ya udugu, umoja na mshikamano, warithi wake walipaswa kuwa na kazi ya kuimarisha mifumo hiyo, kuitetea na kuipalilia. Lakini kazi kubwa zaidi ya warithi wake hao ilipaswa kuwa kwenye eneo la ujenzi wa uchumi imara na unaojitegemea.

  Utawala wa Mwinyi

  Alipoingia Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi mambo yalianza kuharibika na sintofahamu ikawa kubwa. Rushwa ikaanza kuwa mchezo wa kawaida na mfumo wa tajiri kumtawala maskini ukarudi kwa asilimia 100.

  Bahati ya Mwinyi ilikuwa kwamba watu wa kumwambia ukweli na akawasikiliza walikuwapo, mmoja wa watu hao alikuwa Mwalimu Nyerere. Pamoja na kuharibu kwa Mwinyi, walau aliongoza kipindi ambacho Nyerere alikuwa hai na alikuwa na nguvu kubwa ndani ya CCM na serikalini.

  Alipokuja Rais mstaafu Benjamin Mkapa akafunga pingu za maisha na wawekezaji wa kigeni bila mifumo sahihi ya kusimamia ajenda hiyo.

  Pamoja na juhudi za Mkapa kwenye kukuza na kuimarisha uchumi bado alishindwa kuufanya uchumi umilikiwe na Watanzania wenyewe.

  Uchumi wa Mkapa ukakua mikononi mwa wawekezaji. Miaka minne ya mwanzo ya Mkapa naye alipambana na joto la uwapo wa Mwalimu Nyerere, lakini mwaka 1999 Mwalimu akaondoka duniani na kumwachia Mkapa uhuru mkubwa zaidi.

  Mkapa akautumia uhuru huo ipasavyo na miaka sita iliyofuatia akaondoka madarakani na kumkabidhi nchi Jakaya Kikwete.

  Kikwete alikuwa Rais mpole, mcheshi, mtaratibu, lakini mzito kuchukua uamuzi mgumu. Katika uongozi wake nchi iliweka rekodi ya ukopaji. Ikumbukwe kuwa, Mkapa alifanya kazi kubwa ya kulipa madeni ili nchi ianze kujitegemea kiuchumi, alipoingia Kikwete deni la taifa likaanza kupaa kama roketi, miaka kumi ya JK ilipokwisha Tanzania ikawa inadaiwa trilioni 38 hadi 40.

  Wakati huohuo, thamani ya shilingi ya Tanzania ikaporomoka kwa kasi kubwa na tena mfumuko wa bei ukawa juu kupita kiasi. Kikwete alikuwa mtaratibu lakini akishindwa kujenga uchumi imara.

  Ni urais wa Kikwete ndiyo ulimalizia nguvu za mwisho za CCM hadi chama hicho kujikuta kinasaka “mtu’ wa kukiokoa baada ya tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa hakiuziki tena kwa wananchi.

  Ujio wa JPM

  Novemba 2015 aliingia JPM, akikuta bado malengo ya Nyerere hayajatimia, nguzo alizozipanda mwalimu Nyerere zikiyumba.

  Njia nyepesi ya JPM ilikuwa ni kutengeneza uongozi shirikishi (Participatory leadership) kwa ajili ya kuleta maendeleo jumuishi (inclusive development), kusimamia taratibu, sheria na katiba ya nchi katika masuala yote ya msingi, kuzuia mianya ya rushwa iliyokomaa kutoka utawala wa Mwinyi, Mkapa na baadaye Kikwete na kujenga uimara wa taasisi ya Rais na uamuzi wake.

  Kwa bahati mbaya JPM ameshindwa kutengeneza uongozi shirikishi na kujenga Taifa lenye umoja. Kwa maneno yake na vitendo, ameonyesha waziwazi kuwa anachukia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa habari, uhuru wa Bunge na mahakama.

  Kwa maneno na matendo yake amekuwa akizunguka nchini na kutoa matamshi ambayo yanavunja taratibu za kisheria na kikatiba na tena amekuwa akitoa kauli za vitisho na zisizoliunganisha taifa, huu siyo uongozi shirikishi na wala hauwezi kuleta maendeleo jumuishi kama dhana ya juu kabisa ya utekelezaji wa falsafa za maendeleo ya kisasa hapa duniani.

  Utawala wa Kikwete uliwafanya Watanzania watamani kuwa na rais imara na mwenye uwezo wa kufanya uamuzi. Kwa bahati mbaya, Watanzania wamepata rais mwenye uamuzi usiotabirika.

  Tangu JPM aingie madarakani kumekuwa na misuguano baina yake na wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya siasa.

  Misuguano hii inaonekana itapamba moto ikiwa JPM atakosa washauri imara na watu anaoweza kuwasikiliza ndani na nje ya CCM. Utawala wa JPM unaweza kuungwa mkono kwa hatua za kimaendeleo (ikiwa yatakuwa dhahiri ndani ya miaka hii michache), lakini uungwaji mkono huo utategemeana na ikiwa Serikali yake inaacha ukandamizaji wa dhahiri dhidi ya haki za kiraia, vyama vya siasa vya upinzani, vyombo vya habari na Bunge.

  Wazee washauri wapo wapi?

  Wapo watu ambao wanadharau uhuru wa vyama vya siasa, wanakejeli uhuru wa vyombo vya habari na kupuuza uhuru wa Bunge. Watu wa aina hiyo ndiyo wamejazana katika nyadhifa muhimu za uamuzi, ambao wangeliweza kumuokoa JPM na akarudi kwenye mstari.

  Kuna wazee wenye heshima zao na wengine wamewahi kuwa marais wastaafu, hawa pia ilitegemewa wachukue jukumu la kumueleza JPM ukweli, kwamba arudi nyuma na kutafakari kabla Taifa halijawa na matatizo makubwa. Wazee hao nao, kwa bahati mbaya, wameweka vichwa mchangani.

  Katikati ya mgawanyiko huu wa sasa, sioni ni namna gani JPM atapata mwanya wa kulisimamia taifa kufikia malengo aliyokuwa nayo baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

  Ndiyo maana nitakuwa mwongo nikiungana na kundi litakalojaribu kumlinganisha JPM na Mwalimu Nyerere. Hawa ni viongozi tofauti kabisa na hawafanani hata chembe.

  Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, mtafiti na Mwanasheria Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku