Sep 8, 2016

Ni Kinyume Cha Sheria Kwa Mgambo Kuwanyanyasa Wafanyabiashara Wadogo - Jaffo

Jaffo

Serikali imesema ni kinyume cha sheria kwa askari mgambo kuwanyanyasa Mama Lishe na wafanyabiashara wengine wadogo nchini.

Akijibu swali la Mhe. Zaynab Vulu (Viti Maalumu) alilotaka kujua kwanini Serikali isiandae mazingira mazuri ya kufanyia kazi wafanyabiashara hao, Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jaffo amemesema kuwa askari mgambo wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu bila kuwanyanyasa wala kuwadhulumu wakati wakiwaondoa katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Naibu Waziri Jaffo aongeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wafanyabiashara hao walioko katika sekta isiyo rasmi katika kukuza kipato na ajira.Aidha, Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa askari mgambo yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya kuwanyanyasa wafanyabiashara na Mama Lishe wanapotekeleza majukumu yao.

Mbali na hayo, Naibu Waziri amezikumbusha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo Mama Lishe karibu na maeneo walipo wateja wao.

Zaidi ya hayo Naibu Waziri huyo amewataka wafanyabiashara wadogo nchini kufanya biashara katika maeneo yaliyotengwa rasmi na Halmashauri na kuacha kufanya biashara hizo katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Bonyeza HAPA Kudownload Application ya Udaku Special Blog Kwenye Simu Yako

Share:

0 maoni:

Post a Comment

Trending News

Copyright © Siasa Huru | Powered by Blogger Design by JK | Blogger Theme by JR