• Breaking News

  Sep 20, 2016

  SIASA Siasa Zaathiri Misaada ya Tetemeko la Ardhi Bukoba

  Vyama vya siasa; CCM na vile vinavyounda Ukawa hususani Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi vimetia chumvi kwenye kidonda baada ya kuingiza siasa kwenye maafa ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera huku waathirika wakilia kutofikiwa na misaada.

  Wakazi wa maeneo mbalimbali mkoani hapa wanalia kwa kutofikiwa na misaada inayotangazwa huku vyama hivyo vikirushiana lawama kwa kutaka kutumia janga hilo lilisababisha vifo vya watu 17 kujiimarisha kisiasa.

  Mvutano kati ya vyama hivyo ulianza katika hatua za awali za kuwatambua waathirika wa tetemeko hilo katika Manispaa ya Bukoba inayoongozwa na Ukawa ambako CCM ililalamika ikidai wanachama wake wanabaguliwa.

  Naibu Katibu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka aliyeko Bukoba alisema baadhi ya wananchi wamebaguliwa kwa sababu ya itikadi zao na kuwa misaada kadhaa imetolewa ikiwa na nembo za vyama vya Ukawa, jambo ambalo alisema halionyeshi mwelekeo mzuri.

  Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahamud aliwashutumu Ukawa kuwa wanatumia nafasi ya kuongoza manispaa kucheza faulu kwa wanachama wa CCM.

  “Niko hapa Hamugembe, kuna siasa zimeingia katika suala la maafa, Chadema wamekosa ustaarabu, kila eneo wanawafuata wanaogawa misaada na kuwaambia wananchi angalieni tunavyowashughulikia,’’ alilalamika Mahamud.

  Alisema wapinzani wamefika kila eneo unapotolewa msaada na kuwarubuni wananchi kwa kuwa wanaongoza maeneo mengi.

  Naibu Meya wa Manispaa ya Bukoba, Jimmy Karugendo aliitaka CCM na Serikali kuonyesha dhamira yao ya kuwasaidia wananchi kwa vitendo badala ya kulalamika huku wananchi wakiendelea kuteseka.

  “Kama kuna mwenye ushahidi kuwa upinzani tumeshiriki kugawa vitu kwa upendeleo waulete, CCM ndiyo wanatumia maafa kufanya siasa kwa kuvaa nguo zao za chama na kutembelea waathirika wakitangaza siasa,” alisema Karugendo.

  Alisema baadhi ya maturubai kuonekana yameandikwa Ukawa siyo dhambi kwa kuwa msaada huo unasaidia wananchi wote kuwakinga na mvua pamoja na jua bila kujali itikadi zao.

  Alisema ni jambo la kawaida mtoa msaada kuweka maandishi yoyote kwa ajili ya kumbukumbu yake kama ilivyofanyika kwa Msalaba Mwekundu na watu wengine ambao hawahojiwi.

  Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kagera, Gregory Gabone alisema maafa si suala la kujivunia na kutumia kisiasa hivyo ameitaka Serikali ibebe mzigo na kuwa kazi ya wapinzani ni kuisaidia itimize wajibu wake.

  “Hatuna haja ya kutafuta sifa kupitia maafa haya na hatutegemei kujenga chama kwa njia hiyo, ni lazima Serikali iambiwe ukweli, viongozi wote inabidi tujipange na kuangalia jinsi tunavyoshughulikia tatizo hili,’’ alisema Gabone.

  Akizungumzia mvutano huo wa vyama vya siasa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu), Salum Kijuu alisema amekwishatoa maagizo na atahakikisha suala hilo halijitokezi.

  “Mambo ya itikadi za kisiasa nitahakikisha hayajitokezi katika kipindi hiki tunaposhughulikia tatizo la maafa,” alisema Kijuu.

  Kuhusu maturubai yenye nembo za Ukawa, alisema ameshaagiza yaondolewe katika maeneo yote kwa kuwa huo siyo wakati wa siasa.

  Wananchi walalamika

  Kuhusu suala hilo baadhi ya wananchi waliohojiwa wamesema misuguano ya kisiasa ni chanzo cha kutofikiwa na misaada, wakitolea mfano Mtaa wa Nyakanyasi kuwa ugawaji wa misaada umeahirishwa kwa sababu hizo.

  Mjumbe wa Serikali ya mtaa huo, Godfrey George alisema mmoja wa viongozi alitaka hema moja lijengwe kwake licha ya kutopata madhara makubwa, hali iliyosababisha mgawanyiko na utoaji wa misaada kuahirishwa.

  Mkazi wa mtaa huo, Edgar Modest alikosoa msaada unaotolewa kuwa hauendani na uhalisia, akisema pakiti za biskuti wanazopewa haziwasaidii katika kipindi hiki cha dharura.

  Jovinatha Syprian alisema kwa siku saba tangu maafa yatokee, amepata kilo tatu za mchele bila kuulizwa ukubwa wa familia yake na kushauri wenye watoto wasaidiwe dawa za kujikinga na mbu.

  Harambee yakwama Dar

  Itikadi hizohizo zimedaiwa kukwamisha harambee ya kuwachangia waathirika wa tetemeko hilo iliyoitishwa jijini Dar es Salaam na Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare ambaye alisema imefikia hatua wafuasi wa CCM na Chadema wakialikana hawahudhurii hata kama ni masuala yenye masilahi kwa Taifa.

  “Mwanzo nilichukua ukumbi wa watu 100 tu baadhi ya watu wakalalamika na kunishauri kuwa nitafute ukumbi mkubwa zaidi lakini haohao walionishauri nitafute ukumbi mkubwa zaidi leo hawajafika, huenda wanaogopa kuja kwenye shughuli ya mbunge wa Chadema kutokana na itikadi za kisiasa.

  Aliyepagwa kuwa mgeni rasmi, Salum Mwalimu alisema Rais John Magufuli amezuia tetemeko kutumika kisiasa, lakini si kigezo kwamba asikosolewe, hivyo pamoja na majukumu mengi aliyonayo alipaswa kwenda kuwajulia hali waathirika hao kuwapa faraja.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku