• Breaking News

  Sep 13, 2016

  Siri ya Serikali Kushindwa Kupima na Kutabiri Matetemeko ya Ardhi Yabainika


  WAKATI taifa likiwa katika majonzi kutokana na vifo 16 vilivyotokana na tetemeko la ardhi na kuacha majeruhi zaidi ya 253 mkoani Kagera wiki iliyopita, siri ya kushindwa kupimwa matetemeko nchini imebainika.

  Imeelezwa kuwa vituo vitatu vikubwa vya kupima matetemeko   vimefungwa baada ya kuhujumiwa na vingine vidogo 38 navyo vimefungwa baada ya wafadhili kujitoa.

  Hayo yalielezwa  jana na Jiolojia Mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Mbogoni alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

  “Kwa kweli wanajiolojia tunapata changamoto kubwa katika kupima na  kujua iwapo tetemeko litatokea katika eneo fulani na hiyo inatokana na kuhujumiwa  baadhi ya mashine katika vituo vyetu.

  “Tulikuwa na vituo zaidi ya 10 vya kupima matetemeko, hivi sasa  vimebaki tisa pekee  na ili kupata uhakika kama kuna tetemeko kwenye eneo fulani lazima uwe na vituo zaidi ya vitatu,” alisema.

  Alisema vituo vilivyofungwa baada ya   kuibwa  vilikuwa katika mikoa ya Morogoro, Dodoma (Ntuka) na Arusha  eneo la Longido.

  “Ili tuweze kusimika mashine za kupima tetemeko tunahitaji kupata eneo ambalo lina mwamba mgumu.

  “Zamani tulikuwa tukitafuta maeneo yenye miamba migumu huko vijijini, tukipata tunawasiliana na viongozi wa kijiji na tunaweka walinzi wa kulinda mashine hizo.

  “Lakini zimeibwa hali iliyosababisha kufungwa   vituo hivyo…tulipeleka kesi mahakamani mwisho tukaona ni vema sasa tuanze kuzifunga mashine hizo katika maeneo ya magereza kwa usalama wake isipokuwa kile cha Mtwara na Dodoma,” alisema.

  Alisema wezi hao, wamekuwa wakiiba mashine hizo wakidhani  wanaweza kunufaika, wakizifananisha na madini.

  “Wengi wanadhani zinamilikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kwamba wakiziiba watauza wapate faida.  Unajua mashine hizi zipo kama sanduku, wanapoziiba huwa hawawezi kuziuza popote kwa sababu zinatambulika,” alisema.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku