• Breaking News

  Sep 25, 2016

  TATIZO la Lipumba CUF ni Nguvu ya Mvuto ya Edward Lowassa

  Mwanazuoni wa Marekani, Bertram Raven, kupitia maono yake ya kitaaluma, anaweza kunisaidia kuufafanua mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (Cuf).

  Raven ambaye ni profesa mstaafu (professor emeritus) kitivo cha saikolojia, Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, Marekani, mwaka 1959 aliandika dhana tano kuhusu nguvu. Dhana hzo zimekuwa zikitumika katika masomo ya saikolojia, sayansi ya jamii na siasa.

  Katika dhana hizo tano kuhusu nguvu, mojawapo ndiyo ambayo inakitetemesha Cuf. Inawaweka mbalimbali wanasiasa waliokuwa na ushirikiano mkubwa, Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

  Nguvu ya mvuto (referent power) ndiyo ambayo imekigawa Cuf na kutengeneza makundi mawili yaliyopo kwa sasa. Na nguvu hiyo ya mvuto si ya mwingine bali Waziri Mkuu mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa.

  Katika siasa au kwenye jamii yoyote ile, mwenye nguvu ya mvuto ni wa kumuogopa maana husikilizwa yeye tu. Ukishindana naye utaishia kuzomewa hata kama wewe ndiye mwenye hoja za msingi.

  Aliye na nguvu ya mvuto au unaweza kuita nguvu ya haiba, humzidi hata yule ambaye ana nguvu za mamlaka. Ni kwa sababu anapendwa, kwa hiyo neno lake au uwepo wake huwa na kishindo kikubwa. Hii ni kwa sababu ya yale mahaba.

  Kumbukumbu mwaka 1995

  Uchaguzi Mkuu 1995, ulishuhudiwa na nguvu kubwa ya mvuto kwa mgombea urais wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Augustino Lyatonga Mrema. Kujivua kwake uanachama wa CCM na kujiunga kwake na NCCR-Mageuzi, ilikuwa habari kubwa mno kwa upinzani.

  Kipindi ambacho Mrema anajiunga NCCR-Mageuzi, kama angetokea kiongozi yeyote ndani ya chama hicho ambaye angempinga, angeng’oka tu. Hii ni kutokana na nguvu kubwa ya mvuto ambayo alikuwa nayo.

  Hata kama Mrema asingekwenda NCCR-Mageuzi, chama chochote cha upinzani ambacho angejiunga nacho, kama kungekuwa na mtu ambaye angetaka kumzuia asigombee urais, angeondoka yeye na kumwacha Mrema.

  Hivyo ndivyo nguvu ya mvuto inavyofanya kazi. CCM yenyewe ilibaki salama kwa sababu ya uimara wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, vilevile mwamko mdogo wa upinzani uliokuwepo wakati huo.

  Uchaguzi Mkuu 2005, nguvu ya haiba ilikuwa upande wa mgombea urais wa CCM, Dk Jakaya Kikwete, ndiyo maana alishinda kwa kishindo ambacho hakijawahi kutokea.

  Kama CCM ingejaribu kumzuia Dk Kikwete kuwa mgombea urais mwaka 2005 kisha ingetokea naye kutokukubaliana na uamuzi huo, hivyo kutimkia upinzani, chama hicho kingepata msukosuko mkubwa haijapata kutokea.

  Zaidi, Kikwete angehamia chama chochote cha upinzani angeachiwa njia tu ya kugombea urais. Kama angetokea yeyote wa kumpinga, angetoswa yeye kisha JK angejinafasi kwa nguvu kubwa aliyokuwa nayo.

  Katika siasa mvuto binafsi huchochea ushawishi kwa kiwango kikubwa mno. Hata wapigakura wengi huelekea kwenye masanduku ya kura kwa muongozo wa jina, siyo sera. Nguvu ya mvuto ina kawaida ya kushinda kila siku.

  Kishindo cha Trump

  Bado huamini kuwa nguvu ya mvuto hushinda kila siku? Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump, amethibitisha ndani ya chama hicho kuwa haiba yake inashinda uwezo wa mamlaka na nguvu ya vigogo.

  Shangaa leo kuwa Trump ndiye mgombea urais wa Republican ambacho ni maarufu kama Grand Old Party (GOP), wakati vigogo na maveterani wa siasa ambao ni wanachama wa chama hicho hawakumtaka.

  Ushawishi wa wazee na vigogo wa GOP kuwa Trump asipitishwe na chama haukufua dafu, mgombea waliyempendekeza, Ted Cruz hakufanikiwa. Matokeo yake Trump amekuwa mgombea ambaye hana baraka na wakuu wa chama lakini wanachama ndiye wamemtaka.

  Imetokea Trump anaonekana kama jeshi la mtu mmoja ni kwa sababu vigogo wa GOP walimpinga na imebidi wakae pembeni wamwache apite na nguvu yake ya mvuto. Ndiyo maana haikushangaza kwa Trump kuweka rekodi ya kukusanya michango kidogo ya fedha za kampeni kuwahi kutokea katika historia ya chama, ni kwa sababu wenye fedha hawamtaki lakini wanachama walio wengi ndiye chaguo lao.

  Haiba ya Lowassa 2015

  Tathmni ya jinsi ambavyo Lowassa alikitikisa CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, inatoa majibu kuwa kishindo chake kilikuwa kikubwa. Wakuu waliokuwa na mamlaka kwenye chama hawakumtaka, lakini hakuwaacha salama. Alihama na wengi.

  Kama ilivyo kanuni ya mmiliki wa nguvu ya mvuto katika siasa, Lowassa angeamua kujiunga na chama chochote cha upinzani, ilitakiwa apewe nafasi kutokana na ushawishi mkubwa aliokuwa nao na ambaye angemkatalia angepisha yeye.

  Katika pointi hiyo ndiyo maana alipojiunga na Chadema, aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa alijaribu kumpinga lakini matokeo yake alipisha yeye na kumwacha Lowassa akisimama kama mgombea urais, akipeperusha bendera ya chama hicho.

  Uchaguzi Mkuu 2015 ulikuta vyama vinne vya upinzani, Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD, vikiwa vimeunganishwa na utetezi wa Rasimu ya Katiba kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba mwaka 2014. Ushirikiano wao wakauita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

  Makubaliano ya Ukawa yalikuwa kusimamisha mgombea mmoja wa urais, vilevile mbunge na diwani mmoja kwa kila jimbo na kata. Hapo ndipo hasa Lipumba alipoingia kwenye msukosuko wa kisiasa.

  Kutokana na nguvu ya mvuto ya Lowassa, hata Lipumba akiwa Mwenyekiti wa Cuf, alipojaribu kuwashawishi wenzake kwenye chama chake waungane kumkataa waziri mkuu huyo wa zamani, ikiwezekana Cuf kijitoe Ukawa, walio wengi hawakumwelewa.

  Nguvu ya mvuto kama ilivyo desturi yake, ilifanya kazi ndani ya Cuf na sehemu kubwa yenye nguvu ilikubaliana bora kumkosa Lipumba ili Lowassa agombee urais. Na hayo ndiyo matokeo ya Lipumba kujiuzulu kisha kubaki mwanachama wa kawaida.

  Ni haiba ileile ya Lowassa iliyomng’oa Slaa Chadema ndiyo ambayo ilimfanya Lipumba ashindwe kupumzika kifikra mpaka pale alipoamua kujiuzulu uenyekiti wa Cuf. Alitaka kutumia ofisi za Cuf, Buguruni, Dar es Salaam kujiuzulu Agosti, mwaka jana, wazee walimzuia, baadaye akatumia Hoteli ya Peacock kutangaza huo uamuzi wake huo.

  Upepo haujabadilika

  Matatizo yote ya Cuf kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015 na hata sasa, unaweza kuyaweka kwenye jina moja tu; Lowassa. Hakuna zaidi ya hapo, ingawa wenyewe wanaweza kuvurugana na kushutumiana hata kwenye mambo ambayo yapo nje ya muktadha husika.

  Kama Lowassa angebaki CCM hata baada ya jina lake kukatwa katika mbio za kuwania urais mwaka jana, haya yanayoendelea Cuf yasingekuwepo. Amani ya chama ingetamalaki na sasa hivi Lipumba na Seif lao lingekuwa moja, kuudai Urais wa Zanzibar.

  Makubaliano ya Ukawa kusimamisha mgombea mmoja yasingekuwepo, maana yake Cuf isingeathiriwa na Lowassa kujiunga Chadema. Kwa maana hiyo Cuf kingebaki vilevile, zaidi nacho kingekuwa na mgombea wake. Lipumba angedumu na uenyekiti wake.

  Hata baada ya Lowassa kujiunga na Chadema kisha kupata baraka za Ukawa, kama Lipumba angemuunga mkono na kumfanyia kampeni, matatizo yote yaliyopo Cuf leo yasingekuwepo. Nyimbo za Cuf Bara na Cuf Zanzibar wala Cuf Lipumba na Cuf Seif zisingekuwa zinaimbwa.

  Kinachotokea sasa hivi ni ile imani ambayo Lipumba aliyokuwanayo kuwa kipindi kile alishindwa kuwashawishi wenzake wamkatae Lowassa kwa sababu ya jicho la uchaguzi, maana wengi hususan waliokuwa wagombea ubunge na wengine wabunge sasa hivi, waliamini nguvu ya Lowassa ni msaada wa ushindi.

  Kwa mantiki hiyo, Lipumba akadhani mambo ya uchaguzi yamepita, kwa hiyo akili ni tofauti. Amekuta upepo bado ni uleule. Lowassa akili yake ameshaihamishia kwenye Uchaguzi Mkuu 2020 na anawahitaji Cuf bila Lipumba ili apate nguvu.

  Tatizo Lipumba tayari ameshaweka wazi msimamo wake kuwa atakapofanikiwa kukirejesha Cuf kwenye uenyekiti wake, kitakachofuata kwenye Uchaguzi Mkuu 2020, chama chake kitasimamisha mgombea na kwamba hawatamuunga mkono Lowassa.

  Kimsingi suala la Cuf linaumiza vichwa vya wengi. Hata hivyo ukifuatilia asili ya mgogoro wao, utaona kuwa hakuna kitu hasa ndani ya chama hicho ambacho kinawafanya wao kwa wao wasielewane. Chokochoko yote imekuja baada ya Lowassa kujiunga na Chadema kisha kubarikiwa na Ukawa.

  Mwisho kabisa wa kulaumiwa siyo Lowassa, tatizo ni ile nguvu yake ya mvuto. Usizungumzie Cuf peke yake, sasa hivi kata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akigombana na Lowassa, chama hicho kinaweza kupata mtikisiko wa karne.

  CHANZO: Maandishi Genius

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku