• Breaking News

  Sep 6, 2016

  Wapangaji Magomeni Kota, Kuishi Bure Miaka Mitano

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota kukaa kwenye nyumba za serikali miaka mitano bure na baadaye kuzinunua kwa bei nafuu.

  Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiwahutubia wakazi wa Magomeni ambapo amewataka wakandarasi katika kipindi cha miezi miwili waanze kujenga nyumba 644 kwa ajili ya wazee ambao wameteseka baada ya nyumba zao kuvunjwa.

  Ameongeza kusema kuwa ujenzi huu anataka ukamilike ndani ya mwaka mmoja au miezi sita kama ulivyokuwa kwa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kueleza kuwa atafurahi kukabidhi hati kwa wakazi wa Magomeni Kota pindi nyumba hizo zitakapokuwa zimekamilika.

  “Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uzima ili nyumba hizo zikiwa tayari hati nizikabidhi mwenyewe,” alisema Magufuli.

  Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge hasa kwa kutatua mgogoro wa makazi kwa wakazi wa Magomeni Kota.

  “Mheshimiwa Rais ninakushukuru kwa kuwajali wazee hawa wa Magomeni, nami nilitekeleza maagizo yako na kufuatilia mgogoro huu hadi kupata ufumbuzi”, alisema Lukuvi.

  Lukuvi amesema kuwa mgogoro wa Magomeni ulivyokuwa mkubwa ulistahili nguvu ya Mhe. Rais Magufuli, lakini kwa migogoro mingine ambayo ni midogo, hiyo ameishughulikia na ataendelea kuishughulikia ili kero za wananchi kuhusu ardhi ziishe kama alivyoagizwa na Rais.

  Nyumba zilizokuwa Magomeni Kota zilivunjwa mwaka 2009 na wananchi wakaahidiwa kujengewa nyumba ambazo wangeuziwa kwa bei nafuu.

  Lakini kwa takribani miaka mitano nyumba hizo hazikujengwa hali ambayo iliwafanya wakazi hao waishi maisha ya kuangaika.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku