• Breaking News

  Sep 20, 2016

  ZITTO, Kafulila Wamtwisha Mzigo wa Escrow Rais Magufuli

  Wakati Baraza la Usuluhishi la Benki ya Dunia likitoa hukumu ya kutaka Tanesco kuilipa Benki ya Standard Chartered-Hong Kong (SCB-HK) Sh320 bilioni, wanasiasa wawili walioibua sakata hilo bungeni wamechachamaa wakimtaka Rais John Magufuli awafikishe mahakamani wote waliohusika katika sakata la escrow.

  Katika hukumu hiyo, Baraza hilo limeitaka Tanesco kulipa mamilioni hayo ya fedha baada ya mgogoro wa muda mrefu kati yake na Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).


  Uamuzi huo umekuja wakati Serikali ilisharuhusu kufanyika kwa malipo ya Sh306 bilioni kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya sakata hilo kwenda kwa kampuni ya Pan Africa Power Solutions (T) Ltd (PAP).


  Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema katika shauri hilo, shirika hilo liliwakilishwa na mawakili binafsi kutoka kampuni ya uwakili ya Rweyongeza na ndiyo itakayotoa taarifa kuhusu hukumu hiyo.


  Maoni ya Zitto


  Akizungumzia hukumu hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema: “Rais Magufuli awachukulie hatua wote waliohusika kuitia hasara Serikali kwa kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Tegeta Escrow.”


  Alisema benki iliyotumika kupitisha fedha za Tegeta Escrow ndiyo ilipe deni hilo ambalo linatakiwa kulipwa na Tanesco.


  Mbunge huyo aliyeongoza kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuchunguza sakata hilo, alisema Rais Magufuli aitwae mitambo ya IPTL kisheria na kuimilikisha kwa Tanesco kama ilivyopitishwa katika maazimio ya Bunge.


  “Pia wamkamate Harbinder Singh Seth, mmiliki wa PAP na wafuasi wake wote na kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazohusiana na sakata hilo,” alisema.


  Zitto alisema: “Rais Magufuli aamue ama kusimama upande wa Watanzania au Tegeta Escrow.”


  Alisema haiwezekani Tanesco ikaingia hasara kwa sababu ya uchotaji wa fedha za escrow na Rais akaacha kuwachukulia hatua waliohusika.


  Kiongozi huyo wa Chama cha ACT – Wazalendo alisema, “Inasikitisha kuwalipa watu fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kuwapa mitambo ya kuzalisha umeme huku mkiendelea kuwalipa gharama za uwekezaji.”


  Aliongeza, “Sasa mnawalipa Standard Chartered Bank fedha zao kwa mtambo ambao siyo wenu kwa fedha ambazo mngezitoa kwenye akaunti hiyo, lakini sasa mnazitoa Hazina, inasikitisha.”


  Kauli ya Kafulila


  Aliyeibua sakata hilo, David Kafulila alisema hukumu iliyotolewa wiki iliyopita ilitarajiwa kwa kuwa walishaeleza kuwa aliyelipwa fedha za escrow hakuwa mwenye fedha hizo.


  “Leo vinara waliokuwa wakitetea IPTL bado ni vinara katika Serikali ya Magufuli, fedha za escrow hazikuwa za IPTL sasa tunaingia gharama nyingine, Sh300 bilioni ni lazima tufahamu nani yuko nyuma ya mzimu huu wa escrow,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kusini.


  Kafulila aliungana na Zitto kumuomba Rais Magufuli kuwakamata wahusika wote na kuwafikisha mahakamani. “Bunge liombe ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iwekwe wazi kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema.


  Alitaka maazimio yote ya Bunge yatekelezwe kwa kuwa bado mengi hayajatekelezwa.


  “Hii ni hasara kubwa na inatufunga kisheria, lazima tulipe kama ilivyokuwa Dowans walipotushinda tukalipa Dola za Marekani 94 milioni sawa na Sh200 bilioni na hizi tutazilipa iwe kwa uwazi au kwa siri. “Inaumiza sana kwa sababu kodi ya wananchi italipa fedha ambazo zingetumika kutatua matatizo ya wananchi katika kilimo, maji, elimu na maeneo mengine.”


  Alisema Serikali ililipa fedha hizo Novemba 2013 wakati ikijua bado kuna mgogoro. “Kulikuwa na haraka gani kutoa fedha hizo badala ya kusubiri uamuzi wa Baraza hilo,” alisema.


  Kafulila aliwaomba wabunge kuendelea kupambana bila woga ili waliohusika na ufisadi huo wachukuliwe hatua za kisheria.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku