• Breaking News

  Oct 25, 2016

  ESTER Bulaya Aanza Kupangua Gia za Wasirra Mahakamani


  SHAHIDI namba moja wa upande wa wajibu maombi katika kesi namba moja ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo la Bunda Mjini, Estar Bulaya, ameanza kutoa ushahidi wa kutetea ubunge wake katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.


  Katika utetezi wake huo kwenye Mahakama Kuu mjini hapa jana, Bulaya aliulizwa maswali yaliyojikita kwenye ufafanuzi juu ya kutofautiana kwa idadi ya wapigakura waliojiandikisha kwenye hati yake ya ushahidi na idadi iliyojazwa na msimamizi wa uchaguzi katika fomu namba 24(B).

  Bulaya aliyetangazwa mshindi wa kiti cha ubunge katika jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana alianza kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, anayesikiliza shauri hilo katika Mahakama Kuu mkoani Mara.

  Mbunge huyo alihojiwa na mawakili wa upande wa waleta maombi akiwamo Hajira Mungura, aliyemtaka kuieleza Mahakama kwanini fomu ya matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Lucy Msoffe, ilionyesha idadi ya wapiga kura tofauti na kiapo chake.

  Wakili Hajira: Shahidi aeleze Mahakama katika kiapo ulicholeta mahakamani Julai 11, aya ya saba inaonyesha idadi ya wapigakura waliojiandikisha ni 69,369, wakati kielelezo cha ushahidi kilicholetwa mahakamani hapa na msimamizi wa uchaguzi wajimbo hilo, Lucy Msoffe, kinakinzana na idadi ya wapigakura waliopo katika hati yako ya ushahidi huku kikionyesha idadi sahihi ya wapigakura ilikuwa 69,460 tofauti na yako.

  Bulaya: Tarakimu zilizopo kwenye kiapo changu zipo sahihi, mimi sijakosea kuandika idadi ya wapigakura waliojiandikisha 69,369, ndivyo ilivyo, msimamizi ndiyo aliyekosea katika kielelezo 24(B), aliandika idadi ya wapigakura 69,460 ambayo siyo sahihi, ninachokiamini mimi ni kile nilichokiandika katika kiapo changu na siyo vinginevyo.

  Wakili Hajira: Ieleze Mahakama, msimamizi wa uchaguzi alitangaza idadi ya wapigakura waliojiandikisha walikuwa ni wangapi? Kila mgombea alipata kura ngapi hadi alipomtangaza mshindi?

  Bulaya: Mimi sikumbuki idadi waliyopata wagombea wenzangu ninachokumbuka wakati msimamizi anatangaza idadi ya wapigakura waliojiandikisha walikuwa ni 164,794 ambayo ilikuwa imezidi maana alitangaza idadi hiyo ilikuwa ni ya majimbo matatu ambayo ni Bunda Mjini, Mwibala na Bunda Vijijini, ndizo alizomtangazia mshindi wa jimbo la Bunda Mjini lakini niligundua kuwa amekosea, nikamwambia akafanya marekebisho ya kukata hiyo namba.

  Wakili Hajira: Shahidi alieze mahakama, wakati wa msimamizi wa matokeo alipokuwa akifanya majumuisho katika chumba, alikuwa akiwashilikisha kufahamu matokeo ya vituo ili muweze kwenda naye sambamba, mlikuwa mkitumia fomu namba 24(B)?

  Bulaya: Mimi sikuwa na hiyo fomu namba 24(B) tulikuwa tukiangalia katika TV (Sceen) aliyokuwa akitumia msimamizi wa uchaguzi, hivyo mimi kuwa nayo fomu hiyo niliamini kile alichokuwa akikifanya msimamizi.

  Wakili Hajira: Ieleze Mahakama, wakati mnahakiki kura ulisema ulikuwa na wakala wa mgombea wa CCM ambaye ni Janeth Ezekiel, alikwambia alikuwa mahali hapo kwa niaba ya mgombea, Steven Wasira, alikuonyesha kielelezo chochote kinachomuonyesha yuko sahihi mahali hapo au ulishuhudia wakati akiapa?

  Bulaya: Mimi nilimwona Janeth Ezekiel ambaye ni mleta maombi wa tatu na wagombea wengine ndani ya ukumbi wa majumuisho, nilipomuuliza alinijibu yeye ni wakala wa mgombea wa CCM, lakini hakunionyesha barua wala kielelezo chochote kinachomwonyesha kuingia humo, wala sifahamu kama aliapishwa.

  Jaji Chocha alianza kusikiliza kesi hiyo majira ya saa 3:00 asubuhi kisha akaiahirisha saa 10:28 jioni na itaendelea leo kwa shahidi wa pili kwa upande wa wajibu maombi kutoa utetezi wake.

  Shahidi huyo ni msimamizi wa uchaguzi ambaye anatarajiwa kuwasilisha hati ya kiapo chake cha ushahidi.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku