• Breaking News

  Oct 12, 2016

  Hiyo Ndio Siasa. Wanasiasa Hupendana Kwa Maslahi na Huchukiana Kwa Maslahi

  Mwaka 2012, Zitto Kabwe akiwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, alituhumiwa kwa rushwa bungeni.

  Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi ndio waliotoa tuhuma hizo.
  Wabunge wengine wakawa wakali, wakataka Zitto na wabunge wengine waliotuhumiwa wachukuliwe hatua. Wapo waliokasirika kwa sababu hawapendi rushwa, wengine walikasirika kwa maana waliamini mgawo uliwapita pembeni na wenzao wamefaidi.

  Watuhumiwa walikuwa wengi lakini kwa Zitto ilikuwa ni maalum, maana aliweka msimamo wa kutochukua posho bungeni halafu ni kiherehere sana kuusema ufisadi. Watu wakasema: "Kumbe ndio zake hachukui posho lakini anakula rushwa kubwa."

  Zitto aliondoka Dodoma usiku kurudi Dar, hali ya hewa ilikuwa imeshachafuka. Asubuhi yake aliripoti kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na kujieleza jinsi asivyohusika na tuhuma hizo.

  Dk Slaa akamwambia Zitto arudi Dodoma akafanye press conference kwenye ukumbi wa bunge, aeleze kama alivyojieleza kwake.

  Zitto alirudi Dodoma na kujieleza kwa waandishi wa habari.

  Baadaye kamati ya bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo ilibaini kuwa Zitto na wenzake walisingiziwa na kwamba Muhongo na Maswi walilidanganya bunge.

  Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda aliwapa onyo Muhongo na Maswi kutorudia kusema uongo bungeni na kuchafua wabunge.

  NILICHONACHO

  Mtu katuhumiwa kabla hajajibu chochote alikwenda kwa Katibu Mkuu kujieleza. Hiyo ni nidhamu kwa chama. Lazima kujisafisha kwenye chama kwanza.

  Katibu Mkuu baada ya kuridhika aliagiza Zitto arudi Dodoma kuzikabili tuhuma zake kisha akaenda Dodoma kupambana.

  Katika hili nilijionea nidhamu ya Zitto kwa chama chake, vilevile uongozi wenye kukabili matatizo wa Dk Slaa.

  Sikitiko ni kuwa miaka miwili baadae habari ilibadilika. Zitto alipita joto la kufukuzwa chama.

  Mwaka 2014 Slaa alitangaza Zitto sio mwanachama wao na asipewe ushirikiano na chama kokote kwa sababu alikwenda mahakamani kuomba asifukuzwe uanachama.

  Machi 2015 Zitto alitangazwa kutimuliwa kwenye chama na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu. Siku Lissu anatangaza uamuzi huo, Slaa alikuwa pembeni yake.

  Agosti 2015, Dk Slaa alitokeza hadharani na kutangaza kujivua ukatibu mkuu Chadema na kustaafu siasa, kisha akawa mrusha mabomu hatari kwa Chadema katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015.

  Hiyo ndio siasa. Wanasiasa hupendana kwa maslahi na huchukiana kwa maslahi.

  Zitto yupo ACT-Wazalendo, Slaa yupo honeymoon ndefu Canada. Yeye na mkewe Josephine wanasema "Na mtuache tulale."

  Ndimi Luqman Maloto

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku