• Breaking News

  Oct 17, 2016

  Joseph Mungai Aibuka na Kusema "Kikwete Alinitosa ili Kuwafurahisha Walimu"

  Joseph Mungai, ambaye alikuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni wa Serikali ya Awamu ya Tatu, amepinga vikali shutuma kuwa alishusha kiwango cha elimu, badala yake akairushia lawama awamu iliyofuata kuwa ilifanya maamuzi yaliyozorotesha sekta hiyo.

  Mungai, ambaye alikuwa ajibu tuhuma zilizoelekezwa kwake baada ya kustaafu siasa, amesema hata kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete hakutaka kumteua kuendelea kuongoza elimu kwa kuwa alitaka kufurahisha walimu waliokuwa wakimchukia kutokana na kuwabana.

  Mwanasiasa huyo mstaafu pia alipinga shutuma dhidi yake kuwa alifuta michezo shuleni, akisema hahusiki na suala hilo na alichokifanya ni kufuta michango ya mashindano ya Umiseta na Umitashumta na kutoa maelekezo michezo ifanyike nje ya muda wa masomo au mwishoni mwa wiki.

  Mungai aliamua kuweka bayana masuala hayo wakati alipofanya mahojiano na mwandishi Luqman Maloto kuhusu mabadiliko makubwa ya elimu ambayo Serikali ya Awamu ya Tatu iliyafanya, lakini akaelekezewa lawama kuwa ndiye aliyeyafanya bila kushirikisha wadau na kusababisha kuanguka kwa elimu.

  “Kama nilivyosema, nilijisikia vibaya kuona kazi nzuri tuliyoifanya chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa inabomolewa katika mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne,” alisema Mungai alipoulizwa alijisikiaje wakati anaona Baraza la Mawaziri linabadilisha uamuzi ambao waliufanya wakati akiwa Waziri wa Elimu.

  “Nilisononeka sana. Pamoja na utu uzima wangu, sikusikilizwa. Niliwatahadharisha wahusika kuwa matokeo mabaya ya uamuzi huo watayaona baada ya miaka kadhaa. Matokeo yakawa kama nilivyosema. Baada ya mwaka 2007, matokeo ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne yalianza kushuka mwaka hadi mwaka.”

  Mungai alisema katika kipindi hicho idadi ya wahitimu wanaofeli iliongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia kiwango cha juu mwaka 2012 wakati idadi ya waliofeli ilipofikia asilimia 60.

  Alisema hata vyuo vikuu viliendelea na vinaendelea hadi sasa kupokea wanafunzi wasiojua vizuri Kiingereza kutokana na kufuta hata somo walilolianzisha la muundo wa Kiingereza kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu ya sekondari ili kuwaandaa na masomo ya chuo kikuu.

  Mungai hakutaka kumlaumu mtu yeyote aliyeshika wizara hiyo, akisema katika kipindi cha miaka 55, takriban mawaziri 23 wameiongoza, ikiwa ni wastani wa miaka miwili kwa kila waziri na hivyo hakuna aliyepata muda wa kutosha.

  Akizungumzia uamuzi ambao uongozi wake ulifanya wakati huo, Mungai alisema ni kubuni na kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2004 - 2009 uliopanua elimu ya sekondari kuwafikia angalau nusu ya rika lengwa la miaka 14-18.

  “Tulianzisha vyuo vikuu vishiriki vya elimu vya Chang’ombe na Mkwawa kwa lengo la kufundisha walimu kwa ajili ya utekelezaji wa MMES. Upanuaji wa elimu ya sekondari ulipangwa kuendana na upanuaji wa mafunzo ya walimu wa sekondari,” alisema.

  “Najivunia kufuta ada na kuifanya elimu ya msingi kuwa ya bila malipo na ya lazima kwa kila mtoto wa miaka saba hadi 13. Mzazi alibakia na wajibu wa kumpa mtoto wake malazi, mlo na mavazi. Nilipiga marufuku michango yote ya wanafunzi na wazazi wao. Michango ya ujenzi wa shule ni jukumu la wote wenye uwezo wa kufanya kazi; na siyo wazazi wa wanafunzi peke yao.”

  Alisema wakati huo Serikali ilitoa ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi ya Sh10,000 kwa kila mwanafunzi, kutenga fedha kwa ajili ya michezo baada ya kufuta mchango wa Sh1,000 kwa ajili mashindano ya shule.

  Mbali ya MMES, pia aliandaa na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) 2002 - 2006 iliyotoa ruzuku za maendeleo na uendeshaji kwa wananchi wanaojenga na kuendesha shule. Kadhalika, alisimamia kupunguzwa kwa ada ya shule za sekondari za Serikali za kutwa kwa aslimia 50 kutoka Sh40,000 mpaka Sh20,000 na kuongeza ruzuku maradufu ya kuwasomesha sekondari bila ada, watoto wa familia zisizo na uwezo.

  Alisema anajivunia pia kuanzisha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), katika vyuo vyote vya ualimu, kusimamia marekebisho na kuanza kutekeleza mtalaa mpya wa sekondari uliounganisha masomo ya michepuo (ufundi, kilimo, biashara na sayansi kimu) na masomo ya kawaida uliotokana na mapendekezo ya Taarifa ya Mfumo wa Elimu ya Tanzania unaofaa kwa Karne ya 21 (The Tanzania Education System for the 21st Century).

  Alipoulizwa kitu ambacho angetamani kuendelea kukisimamia wakati Serikali ya Awamu ya Nne ikiingia madarakani, Mungai alitaja maboresho ya elimu kwa kutekeleza mtalaa mpya.

  “Lakini Rais Kikwete aliniteua kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye kidogo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

  Niligundua baadaye kuwa lilikuwapo shinikizo la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) nisiteuliwe kuwa Waziri wa Elimu. Sikupendwa na walimu kwa sababu niliwabana mno,” alisema.

  “Wakajibu mapigo kwa kumwambia mgombea urais wa CCM mwaka 2005 (Kikwete) kuwa wanamuunga mkono, lakini Mungai asiwe tena Waziri wa Elimu. Rais Kikwete akaamua kuwafurahisha zaidi walimu kwa kumteua aliyekuwaRrais wa Chama cha Walimu, Mheshimiwa Margareth Sitta kuwa Waziri wa Elimu baada yangu. Hivyo ndivyo siasa ilivyo.”

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku