• Breaking News

  Oct 28, 2016

  Kinachoendelea Kesi ya Ester Bulaya na Steven Wassira


  Mahakama kuu kanda ya Mwanza imepanga Novemba 22 mwaka huu, kutoa hukumu ya kesi ya kupinga ushindi wa mbunge wa jimbo la Bunda mjini Ester Bulaya iliyofunguliwa na wapiga kura wanne wa jimbo hilo Novemba 25 mwaka jana.


  Kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2015 ilifunguliwa na wapiga kura wanne wa jimbo hilo ambao ni Magambo Masato, Matwiga,  Janes Ezekiel na Ascetic Malagila wakipinga matokeo ya kura zilizotangazwa na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo Lucy Msofee.


  Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Oktoba 3 mwaka huu mjni Musoma na jaji Noel Chocha wa mahakama kuu kanda ya Mbeya, baada ya walalamikaji kushinda kesi ya pingamizi za awali katika mahakama ya rufani iliyowapa wapiga kura haki ya kufungua malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi imehitimishwa na ushahidi uliotolewa na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bunda mjini Lucy Msoffe.


  Kabla ya jaji kupanga tarehe ya hukumu, alitoa maamuzi madogo kuhusu hoja za kisheria zilizotolewa na mawakili wawili wa waleta maombi ambao ni Hajra Mungula na Costantine Mutalemwa, waliotaka mahakama hiyo kuruhusu nakala halisi za fomu namba 21B za matokeo ya vituo 18 vya kata ya guta kuingizwa kama nyaraka mpya kwa kutumia kifungu 176 (1) cha sheria ya ushahidi sura ya 6.


  Hoja hiyo ilipingwa na wakili Tundu Lissu anayemtetea Ester Bulaya, Angela Lushagala na Robert Kidando wanaomtetea msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bunda mjini na mwanasheria mkuu wa serikali, waliodai hoja hiyo haina nguvu kisheria kwa mujibu wa kanuni ya 18 ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.

  Kufuatia hoja hizo, jaji Chocha ametoa uamuzi wa kulikataa ombi la mawakili wa walalamikaji akisema mahakama hiyo haina ulazima wa kukubali au kukataa ombi hilo ambapo licha ya kueleza maudhui ya sheria hiyo namba 176( 1 ) cha sheria ya ushahidi sura ya 6, amesema kwasasa hali ilivyo ombi hilo haliwezi kukubaliwa ili lisije likaathiri maamuzi yake ya baadaye.


  Nje ya mahakama, wakili Tundu Lissu anayemtetea mjibu maombi wa kwanza Ester Bulaya pamoja na wakili Costantine Mutalemwa wakazungumzia mwenendo wa kesi hiyo ambayo majumuisho ya hoja za kisheria yatawasilishwa Novemba 4 kwa njia ya barua pepe kabla ya saa 9.30 alasiri. 

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku